Ndege iliyokuwa imebeba watu 11 ilianguka kwenye msitu katikati mwa Cameroon siku ya Jumatano, Wizara ya Uchukuzi ilisema.
Wadhibiti wa trafiki wa anga ‘walipoteza mawasiliano ya redio na ndege’ ambayo baadaye ‘ilipatikana msituni’ karibu na Nanga Eboko, karibu kilomita 150 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Yaounde, wizara ilisema katika taarifa.
Afisa wa wizara hiyo, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema ndege hiyo ilianguka na waokoaji walikuwa wanajaribu kuona ikiwa wataweze kuokoa mtu yeyote.
Ndege hiyo ilikodishwa na kampuni ya kibinafsi, Kampuni ya Usafirishaji wa Mafuta ya Cameroon (COTCO) inayotunza bomba la hydrocarbon linalopita kati ya Cameroon na nchi jirani ya Chad, duru rasmi ziliiambia AFP.
Ndege hiyo, ambayo aina yake na maandishi yake hayakuwekwa wazi, ilipaa kutoka uwanja wa ndege wa Yaounde-Nsimalen kuelekea Belabo, mashariki mwa nchi, taarifa ya wizara ilisema.
Lilikuwa ni janga kubwa la kwanza la anga kuripotiwa nchini Cameroon tangu 2007, wakati ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways iliyokuwa na watu 114 ilipoanguka baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Douala.
Hakukuwa na manususra katika ajali hiyo.
Miaka mitatu baadaye, uchunguzi wa mamlaka ya usafiri wa anga ya Cameroon ulihitimisha kuwa ajali hiyo ilitokana na makosa ya rubani.
Tangu wakati huo, Cameroon imepata ajali ndogo tu za ndege zinazohusisha ndege ndogo za abiria au helikopta.