Shughuli za uokoaji zaendelea nchini Comoro kutafuta manusura wowote baada ya ndege iliyokuwa imebeba watu14 kuanguka katika visiwa hivyo siku ya Jumamosi.
Shirika la ndege la AB Aviation lilisema kuwa ndege yake ndogo aina ya Cessna ilitoweka kwenye rada takriban kilomita 2.5 kutoka ilipoelekea wakati wa safari yake kati ya mji mkuu Moroni na mji wa Fomboni kwenye kisiwa cha Moheli.
“Operesheni za utafutaji… zimeanza kupata mabaki ya ndege hiyo katika eneo la pwani la Djoiezi kuthibitisha ajali hiyo,” wizara ya uchukuzi ya Comoro ilisema katika taarifa.
Serikali ya Comoro ilisema abiria hao 12 walikuwa raia wa Comoro na kwamba marubani wawili walikuwa Watanzania.
Afisa mkuu wa polisi Abdel-Kader Mohamed alisema boti tatu za mwendo kasi zilitumwa kwenye eneo linalokadiriwa kuwa ndege ilianguka “hali ambayo ilituruhusu kukusanya mabaki kutoka kwa ndege na mizigo ya abiria.”
“Tutaendelea na msako. Maadamu hatujapata miili yoyote, kuna matumaini,” aliongeza.
Usaidizi unatolewa kwa familia zilizoathirika katika kisiwa cha Moheli na kisiwa cha Moroni cha Grande Comore.
“Sina matumaini. Kuanzia kesho, tutaanza kuomboleza dada yangu,” Idi Boina, 55, ambaye dada yake alikuwa mmoja wa abiria, aliambia AFP huko Moroni.
Mamlaka ilisema walikuwa wameomba Msaada kutoka eneo jirani linalomilikiwa na Ufaransa la Mayotte.