Ndege ya shirika la ndege la Amerika yakatiza safari yake baada ya abiria kukataa kuvaa barakoa.

Ndege ya shirika la ndege la American Airlines iliyokuwa ikitoka Miami kwenda London ilikatiza safari yake siku ya Alhamisi baada ya abiria mmoja kukataa kuvaa barakoa, shirika hilo la ndege lilisema.

“Ndege ya 38 ya American Airlines iliyokuwa ikisafiri kutoka Miami kwenda London ilirejea katika uwanja wa ndege wa MIA kwa sababu ya mteja msumbufu kukataa kufuata matakwa ya shirikisho,” shirika hilo la ndege lilisema.

Polisi walikuwa wakisubiri uwanjani wakati ndege hiyo aina ya Boeing 777 iliyokuwa na abiria 129 na wafanyakazi 14 ilipotua Miami.

Wakati ndege ilipotua polisi walimkamata abiria huyo kutoka kwenye ndege bila rabsha yoyote, afisa wa polisi aliiambia CNN.

American Airlines ilisema kuwa inasubiri uchunguzi zaidi kumhusu abiria huyo ambaye sasa amewekwa kwenye orodha ya watu wanaozuiwa kusafiri na shirika hilo.

Utawala wa Usafiri wa Anga ulisema mnamo Januari 2021 utazingatia sera ya kutostahimili watu wanaokataa kufuata sheria za shirikisho zinazoamuru watu kuvaa barakoa kwenye safari za ndege za ndani ya Amerika.

Haya yanajiri huku wahudumu wa ndege wakiripoti idadi kubwa ya visa vya matusi na unyanyasaji kutoka kwa wasafiri wanaokataa kuvaa barakoa.