Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israeli, amesema kuwa maafisa wa serikali yake wameafikiana kuhusu mpango wa kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka licha ya mivutano iliyoshuhudiwa dakika za mwisho.
Netanyahu amesema hivi punde kuwa maafisa wa Israel hatimaye wameafikiana kuhusu makubaliano ya kuwarejesha mateka licha ya mivutano iliyoshuhudiwa. Siku ya Alhamisi, Netanyahu aliituhumu Hamas kuwa inajaribu kuzuia mpango huo, tuhuma ambazo zilikanushwa vikali na kundi hilo. Hata hivyo, mkutano wa leo Ijumaa wa Baraza la Mawaziri ndio unatarajia kuidhinisha au la mpango huo wa usitishwaji mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka.
Awali, Netanyahu alikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia ambao ni washirika wake kwenye serikali na wanaopinga kabisa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka.
Kwa upande wake waziri wa usalama wa Israel kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben Gvir alisema Alhamisi jioni kwamba yeye na wanachama wenzake watajiondoa katika baraza la mawaziri iwapo litaidhinisha makubaliano hayo, na kwamba atarejea serikali ikiwa tu vita dhidi ya Hamas vitaendelea ili kufanikisha malengo ambayo amesema hadi sasa hayajafikiwa.
Mara kadhaa viongozi hao wawili wamekuwa wakipinga kabisa hatua zozote za usitishwaji mapigano wakisema kuwa ili kufanikisha zoezi la kuachiliwa kwa mateka, ni lazima kusitisha misaada yote ya kibinadamu inayotumwa Gaza ili kuishinikiza Hamas kusalimu amri.
Baraza la mawaziri la Israel linatarajiwa leo Ijumaa kuamua ikiwa linaidhinisha au la makubaliano hayo, huku Marekani ikitaja kuwa na imani kuwa mpango huo utaanza kutekelezwa kama ilivyopangwa.
Hayo yakiarifiwa, mashambulizi mapya ya Israel yamesababisha vifo vya makumi ya watu huko Gaza huku jeshi la Israel likisema kuwa lilishambulia takriban maeneo 50 katika ukanda huo.