Zaidi ya ngamia 40 wameondolewa kwenye shindano la urembo nchini Saudi Arabia baada ya mamlaka kugundua kuwa ngamia hao walikuwa wamedungwa dawa aina ya Botox inayotumika mara nyingi na binadamu ili kuondoa makunyanzi usoni.
Tamasha la Camel Festival huandaliwa na Mfalme Abdulaziz wa Saudi Arabia na lilianza mapema mwezi huu katika jangwa kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Saudia, Riyadh. Tamasha hilo huwakaribisha wafugaji wenye ngamia warembo kushindana kwa zawadi ya kiasi cha £50m.
Majaji huamua mshindi kwa kuzingatia umbo la vichwa vya ngamia, shingo, nundu, mavazi na misimamo ya ngamia, lakini utumizi wa sindano za Botox na vipodozi vingine vya kuongezea vimepigwa marufuku.
Majaji katika tamasha hilo la mwezi mzima wameweka mkazo dhidi ya kuwaongeza vipodozi ngamia. Majaji walitumia teknolojia maalum ili kubaini iwapo ngamia hao wamedungwa sindano hizo za botox au kufanyiwa marembo mengine, Shirika la Habari la serikali la Saudi (SPA) liliripoti Jumatano.
Mwaka huu, mamlaka iligundua kuwa makumi ya wafugaji walikuwa wamenyoosha midomo na pua za ngamia, walitumia homoni kuimarisha misuli, walidunga dawa ya botox kwenye vichwa na midomo ili kuifanya kuwa kubwa zaidi, sehemu nyingine za mwili zilijazwa mipira na walitumia homoni kunyoosha nyuso zao.
Shindano la urembo la ngamia ndilo kitovu cha tamasha kubwa zaidi ambalo pia hujumuisha mbio za ngamia, mauzo na sherehe zingine.
Tamasha la Camel Festival hutumiwa kuhifadhi nafasi ya ngamia katika mila na urithi wa ufalme wa Bedouin huku nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta ikiendeleza miradi mikubwa ya kisasa.
Tamasha la Ngamia la Mfalme Abdulaziz ndilo kubwa zaidi la aina yake duniani. Ufugaji wa ngamia ni tasnia ya mamilioni ya dola na tamasha kama hii hufanyika kote kwenye kanda.