Kwa ujumla katiba zote duniani huwa zinafanana. Katiba zinaainisha mifumo ya kisheria ya nchi na pia haki za raia wake. Katiba nyingi za mataifa mengi ziliandikwa karne chache zilizopita, lakini zimerekebishwa na kufanyiwa mabadiliko mara kadhaa.
Nchi nyingi duniani zimeandika katiba kama kanuni zao zakuongoza wananchi. Hata hivyo, urefu wa katiba hutofautiana kutoka taifa moja hadi jingine.
Katiba ya India ndio katiba ndefu zaidi duniani ikiwa na maneno 145,385. Nakala mbili za katiba ya India ziliandikwa kwa mkono, moja kwa Kiingereza na nyingine kwa Kihindi.Katiba hizo zimehifadhiwa katika maktaba ya bunge. Mwaka wa 2012, nakala ya toleo la kwanza la Katiba ya India iliyotiwa saini na rais wa kwanza wa India Rajendra Prasad ilinunuliwa kwenye mnada mjini London kwa takriban $188971.86. Katiba ya sasa ya India ilianza kutumika mwaka wa 1950 miaka mitatu baada ya kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.
Taifa la pili kwa udogo duniani, Monaco ina katiba fupi zaidi duniani. Katiba ya Monaco ilipitishwa mwaka wa 1911 na Mwanamfalme Albert I. Ilifanyiwa marekebisho mwaka wa 1962 na Mwanamfalme Rainier III. Kwa hesabu ya maneno, katiba ya Monaco ina takriban maneno 3,814 ikilinganishwa na maneno 145,385 kwenye katiba ya India.
Katiba ya Marekani yenye maneno 7,762 kwa ujumla inachukuliwa kuwa katiba kongwe zaidi duniani ambayo bado inatumika hadi sasa. Katiba hiyo iliandikwa Mei 25 mwaka wa 1787 katika kongamano la katiba mjini Philadelphia na kusainiwa mnamo mwezi Septemba 1787.
Kufikia Desemba 2014, zaidi ya mapendekezo 11,600 ya kurekebisha Katiba yalikuwa yamewasilishwa katika Bunge la Congress tangu 1789. Kufikia sasa, marekebisho 33 ya katiba yameidhinishwa na Congress na kutumwa kwa majimbo ili kuidhinishwa.
Nchi nyingi za Afrika hazikuwa na katiba kabla ya ukoloni, kwa hiyo katiba za mataifa ya Afrika ziliiga katiba za wakoloni wao.
Ila kuna mataifa kadhaa Afrika ambayo yaliunda katiba mpya tofauti na zile zilizoundwa baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni.
Mnamo Februari 1990 baada ya migomo na maandamano makubwa aliyekuwa rais wa Benin Mathieu Kérékou, alilazimika kufanya marekebisho makubwa ya katiba. Kati ya mabadiliko hayo, katiba mpya ilimuondolea rais nguvu nyingi alizokuwa nazo na ikafuta mfumo wa chama kimoja, kuteuliwa kwa Waziri mkuu na kuwepo kwa uhuru wa bunge.
Katiba ya Afrika Kusini ilipitishwa na Mahakama ya Kikatiba tarehe 4 Desemba 1996 na kuanza kutekelezwa tarehe 4 Februari 1997, katiba hiyo imefanyiwa marekebisho mara 17. Katiba ya kwanza kabisa Afrika Kusini ilitungwa mwaka wa 1909.
Rasimu ya katiba ya Kenya iliwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya tarehe 7 Aprili 2010, ikachapishwa tarehe 6 Mei 2010 na kupigiwa kura ya maoni Agosti 4 2010. Katiba mpya ilikubaliwa na 67% ya wapigaji kura na kutangazwa rasmi 27 Agosti 2010.
Nchini Tanzania kumekuwa na msukumo wa kupatikana kwa katiba mpya kwa muda sasa. Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Katiba ya nne na ilipitishwa mwaka 1977. Tangu mwaka huo imefanyiwa marekebisho kadhaa na kumeundwa tume nne zilizolenga kuundwa kwa katiba mpya.
Katiba bora husaidia kuwepo kwa uongozi wa kidemokrasia.kuchochea maendeleo katika mataifa hayo, kufanyika kwa uchaguzi wa huru na wa haki, kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari na wa kujieleza.