Serikali ya jimbo la Zamfara kaskazini-magharibi mwa Nigeria imemsimamisha kazi kiongozi wa kimila wa Kiislamu (emir) baada ya mshukiwa kiongozi wa genge la utekaji nyara kuteuliwa kuwa chifu wa kimila.
Adamu Aliero Yankuzo, anayeshukiwa kuwa kiongozi wa genge, aliteuliwa kuwa chifu wa jamii ya Fulani (Sarkin Fulani) katika eneo la Yandoton Daji siku ya Jumamosi.
Inasemekana kuwa uteuzi huo ulikuja kama sehemu ya makubaliano ya amani na magenge baada ya kukubali kuweka silaha chini.
Lakini wakosoaji wanasema makubaliano kama hayo hapo awali hayakuheshimiwa na magenge ya wahalifu wenye silaha amabo walihusika na mauaji ya kiholela na utekaji nyara kwa ajili ya fidia katika eneo hilo.
Walioshuhudia waliambia BBC sherehe ya kuteuliwa kwake siku ya Jumamosi ilihudhuriwa na maafisa kadhaa wa serikali na mamia ya watu wanaoshukiwa kuwa majambazi.
Raia wengi wa Nigeria wameonyesha mshtuko na hasira kufuatia uteuzi huo.
Wengine wanasema uteuzi huo utahatarisha mapambano dhidi ya magenge yenye silaha.
Serikali ya jimbo la Zamfara sasa imemsimamisha kazi Amiri wa Birnin ‘Yandoto’, ambaye anadaiwa kumteua kiongozi huyo, na pia imejitenga na uteuzi wake.
Katibu wa jimbo la Zamfara, Kabiru Balarabe Sardauna alisema katika taarifa yake kwamba kamati imeundwa kuchunguza hali zinazosababisha hatua ya amiri kumteua kiongozi huyo.
Bw Yankuzo alitangazwa kama mtu hatari na polisi miaka miwili iliyopita lakini hajawahi kukamatwa kamwe.
Polisi walikuwa wamemtuhumu kuwa kiongozi wa genge ambalo liliaminika kuhusika na matukio kadhaa ya utekaji nyara na vifo vya zaidi ya watu 50 katika jimbo la Katsina mnamo 2020.