Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumanne alitoa wito wa kurejeshwa kwa usalama kwa watu waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo wa wanajihadi wa Nigeria, huku mamlaka za mitaa zikifunga kambi na kuwataka watu kurejea kwenye makazi yao.
Zaidi ya watu 40,000 wameuawa na takriban watu milioni 2.2 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano yaliyodumu kwa muongo mmoja kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kati ya jeshi na Boko Haram na tawi lake la Islamic State Mkoa wa Afrika Magharibi (ISWAP).
Wakati wa ziara ya kutembelea kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Maiduguri, Guterres alisifu juhudi za gavana wa eneo hilo kwa maendeleo katika Jimbo la Borno, kitovu cha mzozo tangu 2009. Mamlaka ya Nigeria inapanga kufunga kambi zote za watu waliokimbia makazi huko Borno ifikapo 2026 — lakini mashirika ya misaada yana wasiwasi kuhusu usalama na hali katika baadhi ya maeneo ambako watarejea.
“Hebu tufanye kile tunachopaswa kufanya kuhusu usaidizi wa kibinadamu kwa kambi hizi,” Guterres alisema.
“Lakini tujaribu kutafuta suluhu kwa watu, na suluhisho hilo ni kuwatengenezea mazingira, hali ya usalama, hali ya maendeleo ili waweze kurejea nyumbani kwa usalama na heshima.”
Maafisa wa Nigeria wanasema wanawarejesha tu watu katika maeneo salama, kwa lengo la kuhimiza kuanza tena kwa kilimo na kuwaondoa watu kwenye usaidizi wa kibinadamu.
Guterres pia alitembelea kambi ya muda ya waathiriwa wa wapigano ya kijihadi na kutoa wito wa kuungwa mkono zaidi kwa juhudi za kuwajumuisha tena katika jamii.
Maelfu ya wapiganaji wa Boko Haram na familia zao wamejisalimisha katika miezi ya hivi karibuni.
“Nilishangaa kuona leo katika kituo hicho kwamba wale ambao wamekuwa magaidi, wanataka kujumuika katika jamii na kuchangia katika jamii. Na sera iliyopo hapa ni sera ya maridhiano,” alisema.
Kabla ya kusafiri kwa ndege kuelekea Nigeria, Guterres alikwenda kukutana na watu waliokimbia makazi yao na wakimbizi magharibi mwa Niger asubuhi.
Ziara yake ya kikanda itakamilika Jumatano.