Watu wenye silaha waliwauwa takriban watu 48 katika mashambulizi dhidi ya vijiji vitatu kaskazini magharibi mwa jimbo la Zamfara nchini Nigeria, afisa wa eneo hilo na wakaazi walisema Jumapili.
Maeneo ya Kaskazini-magharibi na katikati mwa Nigeria yamekuwa yakitishwa kwa miaka mingi na magenge ya wahalifu ambao huvamia na kupora vijiji, kuiba ng’ombe na kutekeleza utekaji nyara mkubwa wa wakaazi ili kupata pesa.
“Jumla ya watu 48 waliuawa na majambazi katika vijiji vitatu vya Damri, Sabon Garin na Kalahe vilivyovamiwa Ijumaa alasiri,” alisema Aminu Suleiman, mkuu wa utawala wa wilaya ya Bakura ambako vijiji hivyo viko.
Makumi ya watu wenye silaha wakiwa kwenye pikipiki waliingia katika vijiji hivyo vitatu katika mashambulizi yaliyoratibiwa, wakiwapiga risasi watu walipokuwa wakijaribu kukimbia, Suleiman alisema.
Mashambulizi mabaya zaidi yalikuwa katika kijiji cha Damri ambapo watu wenye silaha waliua watu 32 wakiwemo wagonjwa hospitalini, Suleiman aliambia AFP,
“Walichoma gari la polisi wa doria, na kuwaua wana usalama wawili.”
Vikosi vilivyowekwa katika eneo hilo viliwakabili washambuliaji hao katika mapigano ya bunduki, na kuwalazimisha kuondoka, Suleiman aliongeza.
Abubakar Maigoro, mkazi wa Damri, alisema watu hao wenye silaha walifyatua risasi kabla ya kupora mifugo na chakula.
“Tulizika watu 48 waliouawa katika mashambulizi hayo,” Maigoro alisema.
Hivi karibuni wahalifu hao wameongeza mashambulizi yao licha ya operesheni za kijeshi dhidi ya maficho yao.
Majambazi wanadumisha kambi katika msitu mkubwa, unaozunguka majimbo ya Zamfara, Katsina, Kaduna na Niger.
Katika miezi miwili iliyopita, wameshambulia treni kati ya mji mkuu wa Abuja na mji wa Kaduna na kuwateka nyara makumi ya abiria na kuwaua wanakijiji 100 na kuua dazeni ya wanachama wa vikundi vya walinzi.
Mapema Januari, watu wenye silaha waliwaua zaidi ya watu 200 katika jimbo la Zamfara.
Kwa mujibu wa Mradi wa Data ya Maeneo ya Migogoro na Matukio (ACLED), majambazi waliua raia 2,600 mwaka 2021, ongezeko la asilimia 250 kutoka 2020.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, kamanda wa zamani wa jeshi, amekuwa chini ya shinikizo kubwa la kukomesha ghasia za majambazi kabla ya kuondoka madarakani mwaka ujao ikiwa mwisho wa mihula yake miwili madarakani.
Ghasia hizo zimewalazimu maelfu kukimbilia nchi jirani ya Niger, huku zaidi ya 11,000 wakitafuta hifadhi Novemba, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Maafisa wa Zamfara wanasema zaidi ya watu 700,000 wamefurushwa na majambazi, jambo lililowafanya maafisa hao kufungua kambi nane za kuwahifadhi.