Shirika la dawa za kulevya nchini Nigeria lilisema Jumatano kwamba limeharibu hekta 255 (ekari 630) za mimea ya bangi na kuwakamata watu 13 katika jimbo la kusini magharibi la Ondo.
Upandaji na utumizi wa bangi umeongezeka katika nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni, licha ya kuwa ni kinyume cha sheria.
”Wakala wa Kitaifa wa Kudhibiti utumizi wa Dawa za Kulevya, NDLEA, katika operesheni kubwa iliyochukua siku saba, wameharibu jumla ya hekta 255 za mashamba ya bangi,” msemaji wa shirika hilo Femi Babafemi alisema katika taarifa yake.
Aidha, watuhumiwa 13 walikamatwa na kilo 250 za mbegu za bangi pamoja na kilo 63.85 (za) bangi,” aliongeza.
Babafemi alisema msako huo uliopewa jina la Operesheni Abub, ulifanyika “ndani ya misitu mikubwa mitano” kuanzia Februari 15 hadi Februari 21.
Picha na video mitandaoni zinazoonyesha maafisa wa sheria wakichoma moto mimea ya bangi.
Mkuu wa NDLEA Brigedia-Jenerali Mohamed Buba Marwa aliwataka maafisa ‘kuangalia zaidi mashamba kama hayo katika sehemu yoyote ya nchi.’
Alisema ni agizo la Rais Muhammadu Buhari “kwamba kilimo na mashamba hayo yote… lazima yaharibiwe.”