Mtoto wa rais wa Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba sasa anasema amechoka kusubiri kuwa rais wa Uganda.
Kupitia mtandao wake wa Twitter, Muhoozi alisema hivi karibuni atachukua msimamo kuhusu suala hilo.
Afisa huyo wa kijeshi mwenye umri wa miaka 48 anayehudumu katika oparesheni maalum za kijeshi na mshauri wa rais, alidokeza kuwa Mawaziri Wakuu wa Uingereza na Finland wana umri wa miaka 42 na 37, wakati anakaribia miaka 50 na bado anasubiri kuwa mkuu wa nchi.
“Waziri Mkuu wa Uingereza ana umri wa miaka 42, Waziri Mkuu wa Finland ana miaka 37. Baadhi yetu wanakaribia miaka 50. Tumechoka kusubiri milele. Tutachukua msimamo! Fidel Castro, SHUJAA wangu, alikua Rais akiwa na miaka 32. Ninakaribia kufikia umri wa miaka 49. Kweli sio sawa. Urais wa taifa umekusudiwa kwa vijana. Ni wangapi wanaokubaliana nami kwamba wakati wetu umefika? Inatosha wazee wanaotutawala. Kututawala. Ni wakati wa kizazi chetu kung’ara,” kamanda huyo wa zamani wa UPDF alisema kupitia mtandao wake wa Twitter kabla ya kuwahakikishia wafuasi wake kuwa atawania urais 2026.
“Mmetaka niseme milele! Sawa, katika jina la Yesu Kristo Mungu wangu, kwa jina la vijana wote wa Uganda na ulimwengu na kwa jina la mapinduzi yetu makubwa, nitasimama kugombea Urais 2026!” alisema.
Jenerali Muhoozi, ambaye hivi karibuni amekuwa akiwakosoa waziwazi wanachama wa chama cha babake, chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) ambacho kimekuwa madarakani tangu 1986 wakati Museveni alipoingia Ikulu kupitia vita vya msituni, alidai kuwa hakuna upinzani nchini Uganda.
Ingawa Kainerugaba siku za nyuma amekanusha mara kwa mara madai kwamba ana nia ya kumrithi baba yake mwenye umri wa miaka 78, mmoja wa viongozi waliokaa muda mrefu zaidi barani Afrika, amefurahia kupanda kwa kasi kupitia safu ya jeshi la Uganda.