Si jambo geni kwa nyimbo za wasanii kupigwa marufuku, Dr Congo Jumanne ilikuwa imepiga marufuku nyimbo mbili kuchezwa nchini humo.
Maafisa wa udhibiti wa muziki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) walikuwa wamepiga marufuku nyimbo mbili zinazomshambulia Rais Felix Tshisekedi. Kufikia Jumatano jioni maafisa wa udhibiti wa muziki walikuwa wameondoa marufuku kwa wimbo mmoja “Nini Tosali Te” (kwa lugha ya lingala, ‘’Ni kipi hatukufanya’)
Tume ya Kitaifa ya Udhibiti walikuwa wametoa notisi kwa wakuu wa vyombo vya habari kutocheza nyimbo hizo nchini DRC.
“Kabla wimbo kuchezwa kwenye radio na televisheni lazima upitie Tume ya Udhibiti, watunzi wa nyimbo hizo hawakufuata sheria zilizopo,” alisema Mkurugenzi wa tume hiyo Didi Kelokelo.
Wimbo huo wa , “Nini Tosali Te” (‘ Ni kipi hatukufanya’, kwa lugha ya Lingala) unataofautisha ahadi alizotoa Tshisekedi alipokuwa upinzani na baada ya kuingia uongozini mwaka wa 2019.
Baadhi ya mashairi kwenye wimbo wa wasanii hao MPR unasema ‘Ulituahidi maisha mazuri baada ya Mobutu kuondoka. Mobutu aliondoka lakini hatukupata chochote, Ulisema utarekebisha mambo iwapo Kabila ataondoka madarakani. Kabila aliondoka lakini maisha bado ni magumu.’
Jina la wasanii hao MPR linafanana na jina la chama cha rais wa zamani Mobutu Sese Seko cha MPR.
Mobutu aliondolewa madarakani na Laurent -Desire Kabila mwaka wa 1997 baada ya kuwa uongozini kwa miaka 32. Laurent Kabila aliuawa madarakani mwaka wa 2001 mwanawe Joseph Kabila akamrithi na kuiongoza DR Congo hadi 2019 alipoondoka uongozini baada ya kufanyika kwa uchaguzi.
Wimbo wa pili uliopigwa marufuku ni “Letter to Ya Tshitshi,” ulioimbwa kwa lugha ya kifaransa unasema na rais wa zamani Etienne Tshisekedi na kupinga maisha ya kifahari ya wanasiasa wa nchini humo
Moja wapo wa mashairi kataika wimbo huo unasema, ’Tangu ulipoondoka, mwanao Felix amekuwa rais… Tumebadilisha utawala bila kubadili mfumo.’
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya, katika taarifa yake kwenye Twitter alisema ‘Uamuzi wa kupiga marufuku nyimbo hizo haukutoka kwa serikali, kila mwananchi anaruhusa ya kujieleza, mradi tu maoni yake yaambatane na sheria zilizopo.’
Nchini Tanzania nyimbo kadhaa zimepigwa marufuku ikiwemo wimbo wa Nay Trueboy ‘Mama’ na hivi maajuzi msanii mwingine Vitalis Maembe aliachiwa na polisi kwa dhamana baada ya kukamatwa kwa madai kuwa wimbo wake ’Kaizari’ uliwashutumu viongozi.