Mahakama ya Rwanda imetoa uamuzi wake leo Jumatatu 20 Septemba kuhusu kesi iliyokuwa ikimkabili Paul Rusesabagina.Kwenye uamuzi wa mahakama,Rusesabagina amepatikana na hatia ya kula njama na kuanzisha mashambulio Rwanda mnamo 2018 na 2019 , na kusababisha vifo vya watu tisa.
Rusesabagina alipata umaarufu kote duniani na kuwa shujaa wa wengi baada ya filamu ya “Hotel Rwanda” kuonyesha alivyookoa maisha ya wengi wakati wa mauaji ya halaiki Rwanda 1994.
Filamu ya ‘Hotel Rwanda’ ilimpa umaarufu mkubwa nchini mwake na hata katika mataifa ya nje. Serikali ya Rwanda haikufurahishwa na msimamo wake kisiasa alipoanza kutumia umaarufu huo kupigania mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Nje ya taifa la Rwanda, Paul Rusesabagina alikuwa shujaa aliyependwa na wengi. Mambo yalimbadilkia mnamo Agosti 2020 alipoonekana Rwanda akiwa amevaa sare ya mahabusu akiwa amefungwa pingu.
Polisi nchini Rwanda wanasema Rusesabagina (67) alikuwa ni mhusika mkuu na mfadhili wa kundi haramu liliohusika na mauaji ya halaiki Rwanda. Familia yake ilipinga madai hayo, na kusisitiza kuwa Rusesabagina alikuwa mfungwa wa kisiasa.
“Baba amekuwa akipigania haki, amani na haki za binadamu. Hivi sasa yeye ndio haki zake zinakiukwa.” Mwanawe Rusesabagina Carine Kanimba, alisema.
Paul Rusesabagina alizaliwa mwaka wa 1954, alisomea Thiolojia kwa muda mfupi baada ya kumaliza masomo yake na baadaye kufanya kazi kwenye hoteli moja nchini Kenya na Uswizi.Aliporudi Rwanda 1984, aliajiriwa kuwa naibu meneja mkuu katika hoteli ya Hotel des Mille Collines.
Aprili 1994, wakati mauaji ya kimbari yalipoanza, Rusesabagina alizingirwa ndani ya hoteli ya Mille Collines akiwa na familia yake na mamia ya wageni wengi wao wakiwa wa jamii ya Tutsi kama mke wake. Rusesabagina aliwapa hifadhi na kuwalinda kutoka kwa makundi ya watu waliokuwa wamebeba mapanga tayari kuwaua.
Rusesabagina, kutoka jamii ya Hutu, aliwatuliza wauaji kwa kuwapa pombe na akatumia ujanja wake kupata chakula. Usiku alitumia nambari ya hoteli kutuma kipepesi kutafuta usaidizi kutoka kwa serikali za Ulaya na pia kumfikia Rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton.
Mauji ya kimbari yalidumu kwa takriban siku 100 na kusababisha vifo vya takriban watu 800,000. Rusesabagina alirudi kazini baada ya mauji hayo kukomeshwa ,ila hakufurahishwa na uongozi mpya wa jamii ya Tutsi ulioondoa jamii ya Hutu uongozini.
Rusesabagina alikishtaki chama cha Rwandan Patriotic Front (RPF), hususan kiongozi wa chama Paul Kagame kwa ubabe na kukuza hisia kali dhidi ya Wahutu baada ya watawala wapya kuimarisha nguzo za uongozi wao muda mchache kufuatia mauaji
ya halaiki.
Rusesabagina na viongozi wengine ambao waliamini nafasi ya upinzani wa kisiasa ilikuwa inahatarishwa waliondoka Rwanda mwaka wa 1996 na kuhamia Ubelgiji.
Rusesabagina alikabidhiwa nishani ya US Presidential Medal of Freedom, na akazuru maeneo mengi duniani akizungumzia uovu wa matendo ya binadamu, huku akitumia umaarufu wake kupinga uongozi wa Rais Paul Kagame na chama cha RPF, matamshi yake yaliwachukiza wengi na akapata maadui wengi.
Alishambuliwa na wafuasi wa Kagame maeneo mengi aliyotembela duniani, hata wale aliowapa hifadhi wakati wa mauaji ya halaiki katika hoteli ya Mille Collines walimgeuka na kumshtaki Rusesabagina kwa kufaidika na mateso yao.
Rusesabagina alikuwa na uhusiano wa karibu na makundi ya wanasiasa wa upinzani. Katika video iliyotolewa 2018, alionekana akiunga mkono kundi la National Liberation Front ,kundi linaloaminika kuwa la kigaidi nchini Rwanda.
“Wakati umefika sasa ambapo itatubidi tutumie njia yoyote ile ili kuleta mabadiliko nchini Rwanda, kwasababu njia zote a kisiasa tulizojaribu hazijafaulu” Rusesabagina alisema.
Miaka miwili baadaye, Rusesabagina alipanda ndege akiamini anaelekea Burundi na akajipata akitua Rwanda, alikamatwa na kushtakiwa kwa kuwa adui wa serikali.