Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amemsifia Rais Joe Biden kwa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka. Obama ametaja hatua hiyo kwa ya kizalendo halisi.
kwenye taarifa aliyotuma katika mitandao Obama alisema, “Biden ni mmoja wa marais wa Marekani waliosababisha matokeo mazuri, rafiki yangu wa dhati na mshirika wa karibu. Leo, tumekumbushwa tena kwamba ni mzalendo sana.”
Biden alihudumu kama Naibu Rais wakati wa utawala wa Obama nchini Marekani na katika taarifa hiyo, alikumbuka jinsi walikutana na kuamua kushirikiana.
“Miaka 16 iliyopita, nilipoanza safari ya kutafuta Naibu Rais, nilifahamu wasifu wa Joe Biden katika utumishi wa umma, lakini kilichonifurahisha hata zaidi ni hulka yake,” alielezea Obama.
Aliorodhesha baadhi ya mafanikio ya Biden akiwa uongozini kama kupambana na kumaliza janga la virusi vya korona, kuunda nafasi za ajira, kupunguza gharama ya dawa, kupitisha sheria ya kwanza ya kudhibiti bunduki katika muda wa miaka 30, uwekezaji katika kusimamia mabadiliko ya tabia nchi na kupigania haki za wafanyakazi.
Utendakazi wa Biden kulingana na Obama, unatosha kumsukuma kuwania uongozi tena na kumaliza kazi aliyoanzisha ingawa ameamua kutogombea tena urais.
Alisifia uamuzi wa Biden akisema lazima alitathmini na kutambua kwamba ndiyo stahiki kwa nchi ya Marekani kwani chama cha Democratic kitakuwa katika hatari iwapo kitamkubalia Donald Trump kurejea ikulu na kuwapa wanachama wa Republican udhibiti wa bunge.
“Hatua hii ni dhihirisho la mapenzi ambayo Joe Biden ako nayo kwa nchi hii na mfano wa kihistoria wa kiongozi mkweli ambaye anasikiliza maoni ya watu wa Marekani,” alisema Obama.
Jana Jumapili, Rais Biden alitangaza kwamba anajiondoa kwenye uchaguzi wa urais na kuangazia uongozi katika kipindi kilichosalia.
Ametangaza kumuunga mkono naibu wake Kamala Haris kuwania urais katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.