Oktoba 20, kumbukizi ya mauaji ya Rais wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi

Muammar Gaddafi, Rais wa zamani wa Libya

Ni siku kama ya leo Oktoba tarehe 20 mwaka 2011 ambapo kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi alikamatwa na kuuliwa katika vita vya Sirte. Gaddafi alipatikana katika maficho yake kwenye bomba la maji magharibi mwa mji wa Sirte baada ya msafara wake kushambuliwa na majeshi ya NATO. Gaddafi alikamatwa na kikosi cha Baraza la Mpito la Kitaifa (NTC) na kuuawa muda mchache baadae.

NTC baadae ilidai kuwa Gaddafi alifariki kutokana na majereha aliyopata baada ya mashambulizi ya risasi alipojaribu kutoroka,ila picha za video zilionyesha wapiganaji waasi wakimpiga hadi kumuua.

Muammar Gaddafi alikuwa kiongozi wa vipi kwa raia wa Libya?

Muammar Muhammad Abu Munyar al- Gaddafi, maarufu kama Kanali Gaddafi alizaliwa mwaka wa 1942 na aliiongoza Libya kutoka mwaka wa 1969 hadi 2011. Alizaliwa karibu na mji wa Sirte na kusomea shule ya jeshi ya Royal Military Academy mjini Benghazi.

Muammar Gaddafi aliingia uongozini baada ya kupindua uongozi wa kifame wa Idriss mwaka wa 1969, Gaddafi alileta mabadiliko mengi katika nchi yake ikiwemo kutupilia mbali katiba ya awali na kuligeuza taifa hilo kuwa Jamhuri ya wananchi yaani ‘Jamahiriya’, alikuwa pia mwenyekiti wa Umoja wa Afrika AU kutoka 2009 hadi 2010.

Libya chini ya uongozi wa Muammar Gaddafi

Chini ya uongozi wa Muammar Gaddafi taifa la Libya lilishuhudia maendeleo katika nyanja tofauti ikiwemo elimu, afya, muundo msingi na makazi ambapo fedha zilizotokana na uzalishaji wa mafuta zilitumika kuboresha maisha ya waLibya.

Elimu ya umma ilikuwa bure kwa wote ikiwemo masomo ya msingi, upili na hata chuo kikuu kwa wasichana na wavulana. Huduma za afya zilikuwa bura kwa wote, idadi ya hospitali chini ya uongozi wake iliongezeka kutoka hospitali 700 hadi 3000 katika muongo wa kwanza wa uongozi wake.

Katika uongozi wake alifanya bidii kuwajengea wananchi makazi bora ili kuondoa makazi duni yaliyokuwa mengi katika sehemu za miji, pia mapato ya kila mtu nchini yaliongezeka hadi zaidi ya $ 11,000 ikiwa ni ongezeko la juu la tano barani Afrika.

Mipango mingi ilianzishwa kuwasaidia wajasiriamali na kukuza biashara nchini humo. Septemba 1969, serikali ya Gaddafi ilizindua mpango wa ‘Green Revolution’ ambao lengo lake ilikuwa ni kuongeza tija ya kilimo ili Libya isitegemee chakula cha kuagizwa kutoka nje.

Kwa ujumla kiwango cha maisha cha Walibya kiliboreshwa sana wakati wa utawala wa Gaddafi.

Serikali ya Gaddafi chini ya chama cha RCC iliongeza maradufu mshahara wa chini wa raia na kuanzisha udhibiti wa bei za kisheria, na ikapunguza kodi kwa kati ya asilimia 30 na 40.

Mnamo mwaka wa 1970, sheria ya usawa wa jinsia iliwekwa na kusisitiza usawa wa mshahara kwa jinsia zote mbili.

Mnamo 1972, sheria ilipitishwa kuharamisha ndoa ya wanawake waliokuwa na umri wa chini ya miaka 16 na kuhakikisha kuwa mwanamke anatoa idhini yake kabla kuolewa.

Tripoli, mji mkuu wa Libya

Muammar Gaddafi na makundi ya mapinduzi

Katika miaka ya 80 na 90, Gaddafi kwa ushirikiano na serikali ya Fidel Castro aliyekuwa rais wa Cuba waliunga mkono makundi ya watu waliotaka mageuzi katika nchi zao, kama chama cha Nelson Mandela wa Afrika Kusini na chama chake cha African National Congress na chama cha Palestine Liberation Organisation chake Yasser Arafat.

Kuunga mkono kwa makundi ya waasi katika mataifa tofauti na madai ya kushambulia na kuvamia mataifa mengine barani Afrika kama vile Chad katika miaka ya 70 na 80 na kuunga mkono makundi ya umoja wa Afrika ,makundi ya kutetea haki za wamarekani weusi kulichangia pakubwa kuvunjika kwa uhusiano wake na mataifa ya magharibi.

Mapinduzi ya 2011,’Arab Spring’

Mapema mwaka wa 2011, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka katika muktadha wa ‘Chemchemi ya Kiarabu’ yaani Arab Spring’. Kundi la waasi lililopinga uongozi wa Gaddafi liliunda kamati iliyoitwa Baraza la mpito la kitaifa Februari 2011. Lengo la kundi hilo ilikuwa kuchukua mamlaka ya mpito katika maeneo yaliyoongozwa na waasi hususan baada ya mauji yaliyotekelezwa na vikosi vya serikali na vile vya waasi katika maeneo hayo. Muungano wa kimataifa ulioongozwa na vikosi vya NATO uliingilia kati mzozo huo mnamo mwezi Machi 2011 na kuunga mkono makundi ya waasi.

Mahamkama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa agizo la kukamatwa kwa Gaddafi na wandani wake mnamo 27 Juni 2011. Serikali ya Gaddafi ilipunduliwa baada ya kutekwa kwa mji mkuu Tripoli na vikosi vya waasi 20 Agosti 2011.

Gaddafi alitorokea mji alikozaliwa wa Sirte na kutangaza mji huo kuwa mji mkuu mpya wa Libya mnamo Septemba 1 2011, kutekwa kwa miji mingine na hatimae Sirte na kuuawa kwa Muammar Gaddafi ndio ulikuwa mwisho wa serikali ya Jamahiriya yake Gaddafi.

Walinzi wa kike wa Gaddafi

Katika uongozi wake, Muammar Gaddafi alikuwa akilindwa na kikosi maalum cha wanawake 30. Majeshi hao walichukua viapo vya uaminifu kwa Gaddafi, pamoja na kuweka nadhiri ya ubikira.

Gaddafi aliazimia kuwa kiongozi tofauti kwa kila njia hata katika mavazi na uongozi.

Rais Muammar Gaddafi na walinzi wake

Muammar Gaddafi aliacha mke Fatiha al Nuri na watotot kumi.