Mwanariadha mwenye kasi zaidi barani Afrika Ferdinand Omanyala mnamo Alhamisi alisema atashiriki Riadha za Dunia huko Oregon baada ya kupewa visa katika dakika za mwisho kusafiri hadi Marekani.
Omanyala — mwanamume wa tatu mwenye kasi zaidi duniani msimu huu — atapumzika kwa saa chache tu kabla kushiriki katika mbio za mita 100 zinazoanza Ijumaa huko Eugene, Oregon.
Lakini mwanariadha huyo wa Kenya mwenye umri wa miaka 26 alisema angepanda ndege ya jioni na alikuwa mwingi wa furaha kwa kupata nafasi ya kushindana kwenye mbio hizo baada ya kupata kibali cha kusafiri.
“Changamoto za Visa hukumba Wakenya na watu wote kila siku, katika kesi hii sikuwa tofauti,” Omanyala alisema kwenye taarifa aliyoichapisha kwenye akaunti yake ya Twitter yenye kichwa ‘Oregon Here I Come.’
Hapo awali alikuwa amekata tamaa ya kushindana baada ya kushindwa kupokea visa, akisema hakukuwa na muda wa kutosha wa kuenda hadi Oregon — safari ya saa 24 au zaidi — kabla ya mashindano.
Lakini ataweza kusafiri kwa muda unaofaa na kuwasili Ijumaa asubuhi baada ya kukabidhiwa visa yake katika wizara ya michezo, kocha wa Omanyala Duncan Ayiemba alisema.
“Atakuwa na saa chache za kupumzika kabla ya kushiriki mbio za mita 100, na tunatumai kufuzu kwa nusu fainali na fainali,” alisema.
Timu ya Kenya ilitakiwa kuondoka kuelekea Marekani kwa makundi mawili siku ya Jumatatu na Jumanne, lakini wanariadha kadhaa akiwemo Omanyala hawakupokea visa.
Hakukuwa na maoni kutoka kwa Athletics Kenya, na sababu za kukwama kwa visa hazijajulikana.
Ripoti zimeibuka kuhusu wanariadha kutoka mataifa mengine wanaokabiliwa na masuala ya kupata visa za Marekani.
Waandalizi wa michuano hiyo Oregon22 na World Athletics walisema Jumatano kwamba walikuwa wanafanya kazi kufuatilia maombi ya viza ‘ambayo mengi yametatuliwa kwa mafanikio.’
“Tunaendelea kufuatilia maswala hayo ambayo hayajakamilika ya visa, “walisema katika taarifa, wakibainisha kuwa usafiri wa kimataifa umekuwa na changamoto zaidi kwa sababu ya janga la Covid-19.”
Omanyala ndiye mwanamume wa tatu mwenye kasi zaidi duniani msimu huu nyuma ya Wamarekani Fred Kerley na Trayvon Bromell, akiweka muda wa sekunde 9.85 mwezi Mei.
Septemba mwaka jana, aliweka rekodi mpya ya Kiafrika ya sekunde 9.77, na kumfanya kuwa mtu wa tisa kwa kasi zaidi kuwahi kutokea, nyuma ya Wamarekani wanne na Wajamaika watatu.
Aliliambia shirika la habari la AFP katika mahojiano ya hivi majuzi kwamba alikuwa ameweka malengo yake angalau kufika fainali ya mbio za mita 100 huko Oregon, akilenga muda wa 9.6sec.
Iwapo angeshinda wakati huo, ingekuwa ushindi wa kihistoria kwa mwanariadha wa Kiafrika.
Omanyala amekuwa mwanariadha wa kwanza wa Kenya kufika nusu fainali ya Olimpiki katika Michezo ya Tokyo mwaka jana.
Aliweza kuwakilisha Kenya mjini Tokyo baada ya Athletics Kenya kulegeza uamuzi wa kuwakataza wanariadha wowote waliopigwa marufuku kushiriki mashindano ya kimataifa.
Alikuwa amesimamishwa kushiriki riadha kwa muda wa miezi 14 mwaka wa 2017 na Wakala wa Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Kenya baada ya kupatikana na dawa iliyopigwa marufuku.