Osinachi Nwachukwu alifanyiwa ukatili wa kijinsia na mumewe kabla ya kifo chake – mwimbaji anadai

Osinachi Nwachukwu, msanii wa nyimbo za Injili

Kifo cha mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za Injili kutoka Nigeria Osinachi Nwachukwu siku ya Ijumaa, kimewashangaza wengi, na kuzua mijadala na madai mapya kuhusu ndoa yake.

Mwimbaji huyo, ambaye alitamba na kibao cha “Ekwueme” ambacho kimetazamwa mara milioni 72 kwenye YouTube, alifariki katika hospitali ya Abuja.

Alikuwa mwimbaji mkuu katika Dunamis International Gospel Centre.

Alishirikishwa katika nyimbo kadhaa maarufu za injili kama vile “Nara Ekele” na Mchungaji Paul Enenche wa Dunamis, Abuja.

Familia yake na mumewe, Peter Nwachukwu, ambaye alikuwa meneja wake, bado hawajatoa taarifa kuhusu kifo chake

Walakini, marafiki wa karibu na washirika wameeleza kwamba uhusiano wake tata na mumewe ulisababisha kifo chake cha ghafla.

Siku ya Jumamosi, msanii mwenzake, Frank Edwards, alidai kwamba mwimbaji huyo alikuwa na mume mkatili ambaye alimpiga mara kwa mara kabla ya kifo chake.

Madai kuhusu kifo chake

Frank Edwards alisema kuwa mume wa marehemu mwimbaji huyo alikuwa na tabia ya kumtusi mke wake hadharani, na mara kadhaa alimnyanyasa.

Akisimulia kukutana na mwimbaji huyo, alisema, “Wakati mmoja akiwa studio, mwanamume huyu alimpiga kofi Osinachi akiwa studio kwa sababu tu alitaka kurekodi wimbo huo kwa lugha ya Igbo kinyume na mapenzi ya mumewe.

“Osinachi hangefanya lolote pekee yake”

“Angesema, tafadhali muombe mume wangu.”

“Sikujua uzito wa kile alichokuwa akipitia”

Mwimbaji huyo pia alidai kuwa mumewe alikuwa akidhibiti na angechukua pesa alizopata kutoka kwa kazi yake ya usanii.

Hata hivyo, alisema mwimbaji huyo alikuwa msiri kuhusu yale aliyokuwa akipitia kwenye ndoa yake.

Bw Nwachukwu hakupatikana ili atoe maoni yake.

https://youtu.be/O6hjZ0cVG7Q
Tazama hapa habari kamili