Mwandishi na mwanaharakati wa Uganda Norman Tumuhimbise ni miongoni mwa wanahabari tisa waliokamatwa kwa mawasiliano ya kuudhi, polisi walisema Jumatatu, mwandishi wa pili kuzuiliwa na mamlaka katika miezi ya hivi karibuni.
Tumuhimbise, ambaye anaongoza vuguvugu la The Alternative Movement na jukwaa la mtandaoni la Alternative Digitalk, alitarajiwa kuzindua kitabu cha kumkosoa Rais Yoweri Museveni mnamo Machi 30. Tumuhimbise na wenzake waliripotiwa kuwekwa kwenye gari na maafisa wa usalama waliokuwa na silaha siku ya Alhamisi.
“Polisi walipata malalamiko kuwa kundi hilo lilihusika katika mawasiliano ya kuudhi na kuendeleza matamshi ya chuki,” msemaji wa polisi wa Uganda, Fred Enanga, aliambia AFP.
“Wako na polisi katika Kitengo Maalum cha Upelelezi huko Kireka (kitongoji cha mji mkuu Kampala) huku uchunguzi ukiendelea,” aliongeza, bila kufafanua zaidi.
Wakili wa washukiwa hao Eron Kiiza aliiomba mahakama ya Kampala kuwaachilia huru Jumatatu, akidai kuwa polisi pia wamechukua simu, laptop, vinasa sauti na kamera kutoka kwa wanahabari.
Wafungwa hao ni pamoja na wanahabari watatu wa kike, kulingana na wakili wao Kiiza.
Habari za kukamatwa kwa watu hao zinakuja muda wa mwezi mmoja tu baada ya mwandishi aliyeshinda tuzo ya Uganda Kakwenza Rukirabashaija kukimbilia uhamishoni kufuatia kuzuiliwa kwake kwa tuhuma za kumtusi Rais Museveni na mwanawe.
Rukirabashaija aliwasili nchini Ujerumani mwezi uliopita kutafuta matibabu baada ya kudaiwa kuteswa gerezani katika kesi iliyoibua wasiwasi wa kimataifa.
Umoja wa Ulaya na Amerika ziliingilia kati, zikitaka aachiliwe.
Mashtaka dhidi ya Rukirabashaija yalihusiana na maoni yasiyofurahisha kwenye Twitter kuhusu Museveni, ambaye ametawala Uganda tangu 1986, na mtoto wake Muhoozi Kainerugaba.
Katika chapisho moja alimuelezea Kainerugaba, jenerali ambaye Waganda wengi wanaamini kuwa anajiweka katika nafasi ya kuchukua mamlaka kutoka kwa babake mwenye umri wa miaka 77.
Uganda imeshuhudia msururu wa mikasa inayolenga kukomesha upinzani, huku waandishi wa habari wakishambuliwa, mawakili kufungwa, waangalizi wa uchaguzi kufunguliwa mashitaka na viongozi wa upinzani kunyamazishwa.