Polisi wa kupambana na ghasia wamekusanyika katika maeneo kadhaa katika jiji la Dar es Salaam asubuhi ya leo, kuelekea maandamano ya chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Vyombo vya habari vya ndani, vimeripoti uwepo usio wa kawaida wa polisi na magari ya maji ya kuwasha katika eneo la Ilala Boma na Magomeni katika jiji hilo la kibiashara.
Chadema kilitangaza kitafanya maandamano ya kulaani matukio ya kutekwa watu na mauaji, lakini Jeshi la Polisi lilitangaza kupiga marufuku maandamano hayo.
“Napenda kuwatangazia kuwepo kwa maandamano, kesho tarehe 23, Septemba, 2024 kuanzia saa tatu asubuhi. Yataanzia maeneo mawili, Ilala Boma na Magomeni Mapipa kuelekea viwanja vya Mnazi Mmoja,” alisema mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe siku ya jana.
Vile vile, leo asubuhi Chadema imeandika kwenye akauti yake katika mtandao wake wa X, kwamba Jeshi la Polisi limemkamata Makamu Mwenyekiti wake Tundu Lissu.
Maandamano na mikutano ya hadhara ya kisiasa yalipigwa marufuku kwa muda mrefu wakati wa utawala wa hayati John Pombe Magufuli, na mwanzoni mwa mwaka 2023 mrithi wake Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza ruhusa ya mikutano na shughuli nyingine za kisiasa.