Polisi yahimiza ushirikiano na wafanyabiashara kuzuia uhalifu

Na Josea Sinkala

Kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa vitendo vya uhalifu katika jamii mkoani Mbeya, Polisi imekutana na wafanyabiashara na kuzungumza mambo mbalimbali katika kuhakikisha uhalifu unakomeshwa.

Kwenye mkutano na watu hao, wafanyabiashara katika Soko Kuu la Mwanjelwa Jijini Mbeya wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia, kudhibiti na kutokomeza vitendo vya uhalifu na wahalifu katika Jiji hilo.

Wito huo umetolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Abdi Issango Mei 07, 2024 wakati akizungumza kwenye kikao na viongozi na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mwanjelwa.

Kamanda Issango amesema Jeshi la Polisi linathamini mchango unaotolewa na wafanyabiashara hivyo litaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa katika maeneo yao ya biashara ili kukuza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa la Tanzania kwa ujumla.

Aidha, Kamanda Issango amesisitiza wafanyabiashara hao kufanya kazi kidigitali kwa kuhakikisha wanafunga kamera za usalama (CCTV) kwenye maduka yao ili kuzuia uhalifu na pindi unapotokea kurahisisha kazi ya upelelezi.

Naye, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Andrew Kantimbo, amewataka wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mwanjelwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kwenda kutoa ushahidi mahakamani badala ya kudai kurejeshewa mali zao wakiomba kutoendelea na kesi hali inayosababisha watuhumiwa kuachiwa na kurudi mitaani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Anthony Mkwawa, amewataka wafanyabiashara hao kushirikiana na Polisi Kata waliopo katika maeneo yao ikiwemo kwa kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi (Sungusungu) ambavyo vitafanya doria kwa lengo la kuzuia uhalifu.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wengine Emmanuel Ndanta amepongeza kazi inayofanywa na Jeshi la Polisi hasa ushirikiano toka kwa Polisi na kutoka ofisini kuwafuata wananchi, ushirikiano ambao umesaidia kuzuia vitendo vya uhalifu na wahalifu hasa uporaji na uvunjaji wa maduka.

Mbali na kutoa elimu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limepata nafasi ya kusikiliza kero na changamoto toka kwa wafanyabiashara hao kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa mteja na kuimarisha ulinzi na usalama katika mazingira yao ya kazi ili kutekeleza kwa vitendo dhana nzima ya Polisi kulinda raia na mali zao.