Raia 18 wameuawa katika mashambulizi mawili yanayoshukiwa kuwa ni ya kijihadi magharibi mwa Niger karibu na mpaka wa Mali, serikali ilisema Jumanne.
Shambulio hilo lilitokea Jumapili wakati ‘majambazi wenye silaha’ wasiojulikana wakiwa kwenye pikipiki waliposhambulia lori lililokuwa likisafiri kati ya vijiji katika eneo la Tillaberi, ambalo liko katika eneo la flashpoint ambapo mipaka ya Niger, Burkina Faso na Mali inakutana, ilisema.
Wizara ya mambo ya ndani, katika taarifa yake, ilisema kuwa watu 18 waliouawa, nane kujeruhiwa huku watano kati ya waliojeruhiwa wamelazwa hospitalini katika hali mbaya.
Lori hilo lilichomwa moto, wizara ilisema, na kuwa msako unaendelea ili kuwapata washambuliaji.
Mkazi wa eneo hilo alithibitisha idadi ya waliouawa akisema kuwa 14 waliuawa katika shambulio la lori hilo.
Mbunge wa eneo hilo, ambaye alitoa idadi ndogo zaidi ya watu waliouawa mapema siku hiyo, alisema kuwa gari lililolengwa na washambuliaji lilikuwa likirejea kutoka mji mkuu wa Niger Niamey Jumapili mchana likiwa limebeba abiria kutoka vijiji vinne vya eneo hilo pamoja na mizigo yao.
“Mashuhuda waliripoti kwamba washambuliaji ‘waliwaua karibu wanaume wote waliokuwa ndani ya lori hilo, kabla ya kuchukua vifaa vyao na kulichoma lori,” mbunge huyo alisema.
Tishio la wanajihadi
Makundi yenye silaha yalifanya mashambulizi mengi dhidi ya raia katika eneo hilo mwaka wa 2021, ikiwa ni pamoja na mauaji ya Novemba 2 ya angalau wanachama 69 wa wanamgambo wa kujilinda.
Mnamo Oktoba 2021, washambuliaji waliokuwa wakiendesha pikipiki waliwaua watu kumi katika msikiti mmoja karibu na Tizigorou wakati wa sala ya jioni.
Jumatano iliyopita kilipuzi kiliwaua wanajeshi watano wa Niger kusini magharibi mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa wizara ya ulinzi.
Mlipuko huo ulitokea katika wilaya ya Gotheye ya Tillaberi.
Magharibi mwa Niger kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya wanajihadi, licha ya juhudi za vikosi vya kimataifa vilivyotumwa katika eneo hilo kupambana na waasi hao wa Kiislamu.
Niger, nchi maskini zaidi duniani kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya Umoja wa Mataifa, inabidi ikabiliane na maasi mawili ya wanajihadi.
Niger Imekabiliana na makundi kama vile Islamic State in the Greater Sahara (ISGS) upande wa magharibi, pamoja na Boko Haram na Islamic State West Africa Province (ISWAP) kusini mashariki, karibu na mpaka na Nigeria.
Jirani ya Niger,Mali imekuwa ikijitahidi kuzuia uasi wa kikatili wa wanajihadi ambao uliibuka kwa mara ya kwanza mnamo 2012, kabla ya kuenea hadi Burkina Faso na Niger.
Maelfu ya wanajeshi na raia wameuawa na watu milioni mbili wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo wa Sahel kote, ambao Mali bado ndio kitovu chake.
Ufaransa ilitangaza kuondoa majeshi yake wiki iliyopita kutokana na mzozo kati yake na utawala wa kijeshi wa Mali, ambao ulichukua mamlaka mwaka 2020 na tangu wakati huo umekaidi wito wa kimataifa wa kurejesha utawala wa kiraia kwa haraka.