Search
Close this search box.
East Africa
Kiongozi wa upinzani Nchini Kenya Raila Odinga na Naibu wa rais William Ruto.

Raila Odinga na William Ruto wamekuwa na uhusiano wa upendo na uhasama kwa muongo mmoja sasa, wote wakiwa wamechangia pakubwa katika siasa za urithi wa rais wa pili wa Kenya hayati Daniel Toroitich arap Moi. Kilele cha uhusiano wao ni pale walipohudumu katika serikali ya pamoja baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 Odinga alipomteua Ruto kuwa waziri wa kilimo kabla watofautiane.

Picha ya Januari 06, mwaka 2008 ikiwaonyesha wakati huo wanachama wa ODM – William Ruto na mgombea urais Raila Odinga pamoja na mkewe Ida wakisali kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi (Photo by SIMON MAINA / AFP)

Uchaguzi wa mwaka wa 2002 kumchagua mrithi wa rais wa pili wa Kenya Daniel Moi uliwaweka Raila Odinga na William Ruto upande pinzani.

Katika uchaguzi huo ushindani ulikuwa kati ya marehemu Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta. Ruto akimuunga mkono Kenyatta ambaye alikuwa chaguo la mzee Moi naye Odinga akimpigia debe Kibaki. Upande wa Kibaki hata hivyo ulipata ushindi pengine kutokana na tamko la Odinga kuwa “Kibaki Tosha”

Hata hivyo, Raila alitofautiana na Kibaki mara tu baada ya Kibaki kuunda serikali. Odinga alijikuta akiwa tena upinzani baada ya kukaribishwa na Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa kiongozi wa upinzani wakati huo  na wandani wake William Ruto.

Hadi kufikia mwaka 2007, Uhuru alikuwa amekiwsha anza kufanya kazi na Kibaki na upande wa upinzani uliongozwa na Raila Odinga. Upinzani ulifaulu kupinga kura ya maoni iliyopendekeza rasimu ya katiba mpya iliyojulikana kama the Bomas Draft.

Hatua hiyo ilipelekea uhusiano wa Raila na Ruto kuimarika hata zaidi na Ruto akahakikisha kuwa Raila anajizolea kura nyingi kutoka ukanda wa Rift Valley katika uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka wa 2007.

Kutangazwa kwa Mwai Kibaki kama mshindi katika uchaguzi huo ulipelekea machafuko kushuhudiwa nchini Kenya. Hali hii ilIpelekea serikali ya Nusu Mkate kubuniwa mwaka wa 2008/2013 Mwai Kibaki akiwa rais, Odinga kama waziri mkuu, Uhuru Kenyatta akishikilia ofisi ya naibu waziri mkuu naye Ruto akiwa waziri wa kilimo.

Hata hivyo, hatua ya William Ruto na Uhuru Kenyatta kupelekwa katika mahakama ya Jinai (The Haque) mwaka wa 2011 kwa madai kuwa walichochea machafuko baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007/2008, iliwatenganisha Ruto na Odinga na kuwaunganisha tena Ruto na Uhuru.

Wawili hao waliungana na kuomba kura ya urais mwaka 2013 na 2017 wakiwa katika tiketi moja. Hata hivyo baada ya kushinda mhula wa pili wa uongozi wao, Rais Kenyatta na naibu wake Ruto wakawa kama maji na mafuta huku Rais Kenyatta akimkumbatia kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya kushikana mkono (the Handshake) mwaka 2018

Sasa tunaona marafiki wa zamani Raila Amolo Odinga na William Samoei Ruto wakiwa katika kinyang’anyiro kikali cha kuwania kiti cha Urais mwaka huu 2022. Je mahasimu hawa wa leo wanaweza kugeuka kuwa washirika wa kisiasa tena?

Comments are closed