Rais Donald Trump atangaza ushuru mkubwa kwa mataifa mbalimbali duniani

 

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza ushuru mkubwa kwa mataifa mbalimbali katika kile alichokiita “siku ya ukombozi”, na hivyo kuzidisha hofu ya kutokea kwa vita vya kibiashara duniani.

US President Donald Trump holds a chart as he delivers remarks on reciprocal tariffs during an event in the Rose Garden entitled “Make America Wealthy Again” at the White House in Washington, DC, on April 2, 2025. Trump geared up to unveil sweeping new “Liberation Day” tariffs in a move that threatens to ignite a devastating global trade war. Key US trading partners including the European Union and Britain said they were preparing their responses to Trump’s escalation, as nervous markets fell in Europe and America. (Photo by Brendan SMIALOWSKI / AFP)

Washirika mbalimbali wa Marekani wameguswa na hatua hiyo. Nchi za Umoja wa Ulaya zimewekewa ushuru wa asilimia 20 kwa bidhaa inazouza nchini Marekani, huku China ikiwekewa asilimia 34 na nchi ya kusini mwa Afrika ya Lesotho ikiwekewa kiwango cha ushuru wa asilimia 50.

 

Mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Uingereza, Brazil, Mexico, Australia, Uswisi, Poland na mengineyo yamekosoa hatua hiyo ya Trump huku baadhi yakisema si ishara ya urafiki na yako tayari pia kujibu mapigo. Hata hivyo  utawala wa Trump umesema hautaitoza ushuru wowote mpya Urusi kwa sababu biashara kati ya nchi hizo mbili imepungua maradufu kutokana na vikwazo vya Marekani tangu Moscow ilipoivamia Ukraine.

 

Mapema mwaka huu, Trump aliwaagiza maafisa wake kuandaa mpango wa kile kiitwacho “ushuru wa malipizano” kwa bidhaa zinazoingia Marekani, akitekeleza ahadi yake ya kampeni “ya jicho kwa jicho” kwenye masuala ya biashara ya kilimwengu.

 

Hayo yanajiri wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio anatarajiwa leo Alhamisi kuwasili mjini Brussels-Ubelgiji ambako atashiriki mkutano wa siku mbili wa wanadiplomasia wakuu wa Jumuiya ya kujihami ya  NATO.

 

Ziara ya Rubio itafanyika wakati washirika wa Marekani kwenye muungano huo wa kijeshi wakiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu sera za utawala wa rais Donald Trump hasa kutokana na ukaribu wake na rais wa Urusi Vladimir Putin na hatua zake za ushuru.

 

Kwa miaka 75, NATO imekuwa ikitegemea mwongozo na msaada wa Marekani lakini mambo yamekuwa tofauti tangu kurejea kwa Trump madarakani, huku viongozi wa Ulaya wakihofia hatua za rais huyo wa Marekani wakati wa mkutano wa kilele wa NATO unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni nchini Uholanzi.