Joe Biden ni rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea Angola tangu ilipopata Uhuru 1975 kutoka kwa Wareno.
Rais anayeondoka madarakani nchini Marekani,Joe Biden anaanza ziara yake nchini Angola kuanzia Jumatatu, akitimiza ahadi muhimu aliyoitowa 2022 ya kuimarisha mahusiano na bara la Afrika kwa kuitembelea nchi hiyo.
Biden atakaa mjini Luanda, mji mkuu wa Angola, kuanzia Jumatatu hadi Jumatano ,akiwa rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika yenye utajiri wa mafuta,tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wareno mwaka 1975.
Akiwa Angola anataka pia kuimarisha uwepo wa Marekani katika bara hilo katika kiwingu cha kuongezeka kwa uwekezaji unaofanywa na China.
Rais Biden ambaye kwa sasa hana maamuzi makubwa, wakati anajiandaa kumkabidhi madaraka Donald Trump Januari 20, alipanga mwazoni kufanya ziara yake hiyo mwezi Oktoba lakini ilisogezwa mbele kutokana na kimbunga Milton kilichopiga katika jimbo la Florida.
Hata hivyo afisa mmoja mwandamizi katika serikali ya Marekani amesema ziara hii ya Biden bado haijachelewa.