Baada ya kuwafuta kazi ghafla mawaziri wake wote kwa madai ya ufisadi, Rais wa Malawi Lazarus Chakwera aliwateua tena mawaziri wa awali katika baraza jipya la mawaziri siku ya Jumatano.
Chakwera alifuta baraza lake lote la mawaziri 33 siku ya Jumatatu, na kuahidi “kukabili aina zote za uvunjaji wa sheria wa maafisa wa umma.”
Orodha ya uteuzi wa mawaziri 12 iliyotolewa na ofisi yake baada ya saa sita usiku Jumatano inajumuisha mawaziri wawili wapya pekee, wengine wote ikiwa wale waliokuwa wamesimamishwa kazi.
Mfanyabiashara maarufu na mwanasiasa Mark Katsonga Phiri anakuwa waziri wa biashara, huku mfuasi wa chama tawala Sam Kawale akichukua nafasi ya waziri wa ardhi.
Kawale anachukua nafasi ya Kezzie Msukwa, aliyekamatwa mwezi uliopita kwa rushwa. Mawaziri watakaosimamia wizara za fedha, ulinzi na mambo ya nje bado hawajatangazwa.
Takriban miaka miwili tangu aingie madarakani, Chakwera amekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa makundi ya kiraia na kidini kulichukulia hatua baraza lake la mawaziri, baada ya mawaziri wake kadhaa kukumbwa na kashfa za ufisadi.
Uamuzi wake wa kulifuta baraza lote ulifuatia mikutano iliyofanyika wiki iliyopita kati yake na Baraza la Maaskofu na Kamati ya Masuala ya Umma, ambayo inajumuisha vikundi vya makanisa na vitengo vya serikali.
Mashirika hayo yameeleza kusikitishwa na hali ya rais kutofanya maamuzi dhabiti katika kupambana na ufisadi.
Chakwera alishinda uchaguzi wa urais wa 2020 na ahadi za kupambana na ufisadi nchini mwake.
Mnamo Desemba 2021, uchunguzi dhidi ya rushwa ulihakikisha kuwa waziri wa fedha wa Malawi na gavana wa zamani wa benki kuu wanakamatwa kwa madai ya kupata pesa kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa kwa njia za ulaghai.