Rais Paul Kagame wa Rwanda Ijumaa 24 alianza ziara rasmi ya siku mbili nchini Msumbiji alikotuma kikosi cha wanajeshi 1000 kusaidai jeshi la Msumbiji kukabiliana na wanamgambo wa jihadi.
Mwezi Julai, Rwanda ilikuwa taifa la kwanza Afrika kutuma jeshi lake kusaidia lile la Msumbiji kukabiliana na wanamgambo waliovamia eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Cabo Delgado.
Kagame aliwasili mkoani Pemba Ijumaa asubuhi.
Kati ya shughuli zake nchini Msumbiji ni kukutana na jeshi na polisi waliotumwa kuweka amani nchini humo.
Majeshi ya kigeni, yameisaidia Msumbiji kukabiliana na makundi ya wanamgambo katika mji wa Palma mwezi Machi, makundi yaliyokuwa yakihatarisha miradi ya gesi ya mabilioni ya dola na kuzua wasiwasi wa kimataifa.
Kando na jeshi la Rwanda, mataifa 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pia wamekuwa wakituma majeshi yao ikiwemo majeshi wengine 1,500 ambao Afrika Kusini imeahidi kutuma Msumbiji.
Wakati huo huo Jumuiya ya Ulaya imeanzisha ujumbe wa kijeshi utakaofundisha vikosi vya kijeshi vya Msumbiji kukabiliana na wanamgambo.
Wapiganaji wa Jihad wamekuwa wakifanya uharibifu Cabo Delgado tangu 2017, wakivamia vijiji na miji katika juhudi zao za kutaka kuanzisha himaya ya kiislamu.
Mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,306 wengi wao ikiwa ni raia, na kuwafurusha wengine 800,000 kutoka majumbani mwao katika kipindi cha miaka minne iliyopita.