Rais wa Iran Ebrahim Raisi amethibitishwa kuangamia kwenye ajali ya ndege aina ya helikopta aliyokuwa ameabiri pamoja na waziri wake wa masuala ya nchi za kigeni na wengine.
Ndege hiyo ilianguka katika eneo la milima na misitu na vifo hivyo vilithibitishwa baada ya waokoaji kuweza kupata mabaki ya ndege hiyo na kuripoti kwamba hakukuwa na ishara ya uhai katika eneo la ajali.
Raisi wa umri wa miaka 63 mwakilishi wa mirengo ya kihafidhina na yenye misimamo mikali katika siasa za Iran amekuwa rais kwa karibu miaka mitatu na alikuwa anatarajiwa kuwania tena wadhifa huo mwaka ujao.
Jaji mkuu huyo wa zamani wa Iran alikuwa anatizamiwa kuchukua mahala pa Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi mkuu wa Iran siku za usoni.
Ebrahim Raisi alizaliwa katika eneo la kaskazini mashariki wa Iran linalokaliwa na waisilamu wa Shia na alisomea masomo ya dini ambapo alinolewa na wasomi tajika mmoja wao akiwa Khamenei.
Amekuwa mwanachama wa kundi linalofahamika kama âTwelver Shia Muslimsâ ambalo linaamini kwamba ma imam walikuwa 12 baada ya kifo cha mtume Mohamed na ambao hujitambulisha kwa kuvaa kitambaa cha rangi nyeusi kichwani sawa na anachovaa Khamenei.
Raisi alipata tajriba kama mwendesha mashtaka kabla ya kuhamia jiji kuu la Tehran mwaka 1985 na katika jiji hilo akawa mwanachama wa kamati ya majaji ambayo ilihusika katika kusimamia utekelezaji wa adhabu ya kifo dhidi ya wafungwa wa siasa, kulingana na mashirika ya haki.
Alikuwa pia mwanachama wa kundi la wataalamu lililotwikwa jukumu la kuchagua kiongozi mkuu wa Iran iwapo aliye mamlakani atafariki.
Mwaka 2014 alichaguliwa kama mwanasheria mkuu wadhifa alioshikilia kwa muda wa miaka miwili na baadaye akachaguliwa kuongoza shirika la misaada la Astan Quds Razavi.
Marehemu Raisi aliwania urais kwa mara ya kwanza mwaka 2017, akashindwa na rais Hassan Rouhani aliyechaguliwa kwa muhula wa pili.
Alitulia kwa muda baada ya uchaguzi huo kabla ya kuteuliwa na Khamenei mwaka 2019 kuongoza idara ya mahakama ambapo alijiwasilisha kama mtetezi wa haki naambaye alikuwa anapambana na ufisadi. Alizuru mikoa mbali mbali wakati huo na akapata uungwaji mkono.
Alichaguliwa kuwa Rais mwaka 2021 kwenye uchaguzi ulioghubikwa na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza na kupigwa marufuku kwa wawaniaji kadhaa.
Raisi ni mmoja wa viongozi ulimwenguni waliozungumza dhidi ya hatua ya Israel ya kushambulia wapalestina huko Gaza na akahimiza jamii ya kimataifa kuingilia kati.
Alikuwa ameahidi kulipiza kisasi dhidi ya Israel baada ya Israel kushambulia ubalozi wa Iran nchini Syria ambapo wanajeshi saba waliuawa wakiwemo wakuu wa jeshi wawili.