Rais Ruto Na Raila Wajibizana Kisa Eti Kufunguliwa Kwa Sava Za Tume Ya Uchaguzi.

Miezi saba baada ya matokeo ya urais kutangazwa na aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC Wafula Chebukati,majibizano kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani yamezuka,mara hii yakijikita katika sava za IEBC.


Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ameonekana kusisitiza kuwa uchaguzi huo mkuu ulihitilafiwa kwa kuibiwa Kura,Odinga akidinda kumtambua William Ruto kama rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya.


Katika mikutano ya kisiasa ya hivi majuzi,Odinga ameitaka tume ya huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC kufungua sava zake ili kuonyesha wazi idadi kamili ya Kura zilizopigwa kwa kile mwaniaji aliyekuwa debeni katika uchaguzi huo wa Agosti 9 2022.


Hata hivyo Rais William Ruto amemjibu Odinga kwa kusema kuwa sava za IEBC zilikuwa wazi tangu kusajiliwa kwa wapiga kura,kupiga kura,kutangazwa kwa matokeo na hata wakati kesi ilipoamuliwa na mahakama ya upeo.


“Sava za tume ya uchaguzi zilifunguliwa katika vituo vyote vya kupigia kura kuanzia wakati wa kusajiliwa kwa wapiga kura,ni ukweli kuwa wakati matokeo yalikuwa yanatangazwa pia yalikuwa kwenye sava ambazo zilikuwa wazi.Na hata sava hizi zilisalia wazi wakati upinzani ulipeleka kesi katika mahakama ya upeo,” alisema rais Ruto.


Kulingana na Rais Ruto,kiongozi wa upinzani Raila Odinga anawapotosha wakenya kuwa kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi mkuu 2022.


“Usijaribu kuwapotosha wakenya kwa kusema sava zifunguliwe na zipo wazi.Kugeuka na kujifanya haujui kama sava zimefunguliwa ni kama kutuchukulia wajinga.Nataka nimnukuu mwanamuziki Bob Marley ambaye wakati mmoja alisema unaweza wadanganya watu wote kila wakati ila hauwezi wadanganya watu wote kwa muda mrefu” alisema rais Ruto


Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amezidi kushikilia kuwa kuwa alishinda kiti cha urais katika matokeo ya uchaguzi Agosti 9 kwa kuzoa kura milioni 8.1 dhidi ya milioni 5.9 za Rais William Ruto kulingana na mfichuzi wa siri.