Rais Samia Suluhu Hassan akutana na Tundu Lissu mjini Brussels

Rais Samia Suluhu wa Tanzania hatimaye amekutana na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu kwa mara ya kwanza tangu aende uhamishoni.

Lissu, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alifanya mazungumzo na Rais Samia mjini Brussels, Ubelgiji, Jumatano.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, Dar es salaam, wawili hao walijadili mambo kadhaa.

“Rais Samia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kiongozi wa CHADEMA Lissu walijadili masuala mbalimbali yenye maslahi kwa nchi ya Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.

Rais Samia yupo nchini Ubelgiji baada ya kuhudhuria mkutano uliokutanisha Umoja wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (OACPS).

Kikao hicho kilifanyika Jumanne Februari 15, 2022.

Juni mwaka jana, Lissu alisema yuko tayari kurejea nchini kwake iwapo tu rais atashughulikia jaribio lake la mauaji.

Akizungumza na Ripota wa Mwanzo TV jijini Nairobi wakati wa uzinduzi wa kitabu chake kiitwacho, Parliament and Accountability in East Africa mwaka wa 2021, Lissu alisema kwamba tayari alikuwa amempigia simu rais Samia na kuomba kufanya mkutano naye.

Tazama mahojiano hayo kamili:

https://www.youtube.com/watch?v=7lppj2oTKYE&t=77s

Lissu alishawahi kusema kuwa jaribio lake la kukutana na Samia kupitia kwa katibu wake Juma Mkomi halikuzaa matunda.

Gari la Lissu lilipigwa risasi Septemba 2017 baada ya kutoka nje ya Majengo ya Bunge na kumsababishia majeraha makubwa.

Tukio hilo lilitokea wakati wa uongozi wa hayati Rais John Magufuli. Lissu alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Magufuli, akimlaumu kwa kukandamiza haki za viongozi wa upinzani pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Tanzania.

Hata hivyo alirejea nyumbani mwaka 2020 kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa mwaka huo ambapo chama chake cha CHADEMA kilishindwa na CCM ya Magufuli.