Mahakama ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ICJ, imeamua kwa kiasi kikubwa kuipendelea Somalia katika mzozo wa muda mrefu na Kenya kuhusu mpaka wao wa bahari Hindi.
Kenya iliishutumu Mahakama ya Haki ya Kimataifa kwa upendeleo na ikasema haitakubali uamuzi uliotolewa Jumanne 12. Kesi hiyo inahusu sehemu ya 38, 000 sq ya bahari Hindi inayoaminika kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.
Katika uamuzi wake mahakama imependekeza msitari mpya, ikigawa katikati, sehemu yenye ugomvi na hivyo Kenya ikapoteza sehemu ya eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita 100,000 mraba.
Jopo la majaji 14 wa mahakama ya Umoja wa Mataifa ICJ, katika kikao chake mjini The Hague Uholanzi, siku ya Jumanne walifanya uamuzi huo ambao Kenya imesema haitakubali.
Kenya inasisitiza kuwa msitari uliochorwa kuelekea mashariki kutoka eneo lililo karibu na Lamu, ambapo kuna mpaka wa Kenya na Somalia, ndio mpaka unaotambulika. Somalia nayo inasema mpaka wake unastahili kuwa mstari mstatili jinsi mpaka wake wa ardhi ulivyo.
Mzozo huo wa mpaka kati ya Kenya na Somalia umekuwa kiini cha hali tete ya kiplomasia kati ya mataifa hayo mawili kwa zaidi ya miongo minne.
Kenya na Somalia mapema 2009 zilikuwa zimekubaliana kupata suluhu ya mzozo huo kwa kufanya mazungumzo, Umoja wa Mataifa uliunga mkono pendekezo hilo.
Ila miaka mitano baadae, Somalia ilienda kwa mahakama ya ICJ baada ya mazungumzo kugonga mwamba. Somalia ilikasirishwa na uamuzi wa Kenya kuuza leseni za kuchimba mafuta kwenye eneo linalogombaniwa mwaka wa 2012.
Kenya imeishutumu mahakama ya ICJ kwa kuipendelea Somalia na kwamba haitakubali uamuzi uliotolewa.
Mahakama ya ICJ haina nguvu za kutekeleza uamuzi wowote kuhusu mzozo huo.