Rais wa Burkina Faso Kabore azuiliwa katika kambi ya kijeshi

Roch Kabore, Rais wa Burkina Faso

Rais wa Burkina Faso Roch Kabore amezuiliwa katika kambi ya kijeshi na wanajeshi walioasi, vyanzo viwili vya usalama na mwanadiplomasia wa Afrika Magharibi alisema Jumatatu. Kulikuwa na milio ya risasi kuzunguka makazi yake Jumapili usiku katika mji mkuu Ouagadougou.

Magari kadhaa ya kivita ya rais, yakiwa yameshambuliwa kwa risasi, yalionekana karibu na makazi ya rais Jumatatu asubuhi gari moja likiwa na damu. Wakaazi wanaokaa katika mtaa mmoja na rais waliripoti milio mikubwa ya risasi usiku kucha.

Serikali ilikuwa imekanusha uvumi siku ya Jumapili kwamba mapinduzi yalikuwa yakiendelea huku milio ya risasi ikisikika kwa saa kadhaa kutoka katika kambi tofauti za kijeshi. Wanajeshi waaasi wanadai kuungwa mkono zaidi kwa mapambano yao dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu.

Hali ya wasiwasi imeongezeka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na mauaji ya mara kwa mara ya raia na wanajeshi yanayofanywa na wanamgambo hao ambao baadhi yao wana mafungamano na Islamic State na al Qaeda.

Waandamanaji walikuwa wamejitokeza kuwaunga mkono waasi siku ya Jumapili na wavamia makao makuu ya chama cha kisiasa cha Kabore.

Serikali ilitangaza amri ya kutotoka nje kutoka 2000 GMT hadi 0530 GMT hadi ilani nyingine itakapotolewa, shule zimefungwa kwa siku mbili.