Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi alisema Jumapili ‘hakuna shaka’ kwamba Rwanda inaunga mkono uasi katika eneo lao, lakini akasisitiza kuwa bado anatafuta uhusiano wa amani na Kigali.
Matamshi yake yalikuwa matamshi ya hivi punde dhidi ya kuzuka upya kwa waasi wa M23 wanaoendesha harakati zao mashariki mwa nchi hiyo, karibu na mpaka na Rwanda.
“Siku zote nimekuwa nikisisitiza kwamba unapaswa kujenga madaraja badala ya kuta,” alisema Tshisekedi kwenye televisheni ya taifa, katika matamshi yake ya kwanza ya hadhara juu ya mzozo unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili.
“Kwa bahati mbaya, leo, tuko hapa tulipo.”
Majirani wa DR Congo hawapaswi kufikiria kuwa hamu yake ya kuwepo kwa amani ni udhaifu kwao, aliongeza.
“Hiyo haitoi fursa kwa majirani kuja kutuchokoza,” alisema
“Natumai Rwanda imejifunza somo hili, kwa sababu, leo ni wazi, hakuna shaka, Rwanda imeunga mkono M23 kuja kushambulia DRC.”
Tshisekedi alikuwa akizungumza alipotembelea jirani ya Magharibi ya Kinshasa, Congo-Brazzaville, kwa mazungumzo na Rais Denis Sassou Nguesso.
Kinshasa imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, ambao wamehusika katika mfululizo wa mapigano na jeshi tangu mwishoni mwa mwezi Mei, madai ambayo Kigali imekanusha.
Kinshasa imesitisha safari za ndege za shirika la ndege la Rwanda RwandAir kati ya nchi hizo mbili na kumwita balozi wa Rwanda ili kumuonya kuhusu msimamo wa nchi hiyo.
Uhusiano kati ya DRC na Rwanda umekuwa mbaya tangu Wahutu wa Rwanda wanaotuhumiwa kuwaua Watutsi wakati wa mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994 kufika kwa wingi mashariki mwa DRC.
Uhusiano huo ulianza kuimarika baada ya Rais wa Congo Felix Tshisekedi kuchukua madaraka mwaka wa 2019 lakini kuzuka upya kwa hivi majuzi kwa ghasia za M23 kumezua mvutano wa kikanda.
Wapiganaji wa M23 waliiteka Goma mwaka wa 2012 kabla ya jeshi kuwafukuza kutoka mji huo na kumaliza uasi wao.
Hata hivyo, wanamgambo hao walizuka upya mwishoni mwa 2021 baada ya kuishutumu serikali kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ya 2009 ambayo yalilenga kuwajumuisha wapiganaji wake katika jeshi.