Rais wa Equatorial Guinea Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, ambaye ametawala nchi yake kwa miaka 43, alizindua azma yake ya kuwania muhula wa sita Alhamisi katika hafla ya kwanza ya kampeni.
Obiang, mwenye umri wa miaka 80, aliingia madarakani katika mapinduzi ya mwaka 1979 na ndiye kiongozi wa nchi aliyetawala kwa muda mrefu zaidi duniani ukiondoa wafalme. Hajawahi kuchaguliwa rasmi kwa chini ya asilimia 93 ya kura.
Chama chake kikubwa cha Democratic Party of Equatorial Guinea (PDGE) kilianza kampeni yake ya uchaguzi wa urais, wabunge, seneti na serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 20 katika mji wa kaskazini wa Ebebiyin karibu na mpaka na Cameroon.
Obiang aliwaambia mamia ya wafuasi wake kwamba chama chake kimemchagua kuwania akidai yeye ni ishara ya amani inayotawala guinea ya Ikweta.
Ilani yake ya uchaguzi inatokana na mwendelezo na kuendeleza taifa hilo la Afrika ya Kati, ambalo lina rasilimali kubwa ya mafuta na gesi lakini wananchi walio wengi wanaishi chini ya mstari wa umaskini.
“Rafiki wa zamani ni bora kuliko mpya,” aliongeza naibu na mtoto wa rais, Teodoro Nguema Obiang Mangue.
PDGE inashikilia viti 99 kati ya 100 katika baraza la chini la bunge linalomaliza muda wake na viti vyote vya seneti. Lilikuwa vuguvugu moja la kisiasa la kisheria nchini humo hadi mwaka 1991, wakati siasa za vyama vingi zilipoanzishwa.
Anayewania kiti hicho dhidi ya Obiang ni Andres Esono Ondo wa chama cha Convergence for Social Democracy na Buenaventura Monsuy Asumu, ambaye anawakilisha chama cha Democratic Social Coalition.
Zaidi ya wapiga kura 425,000 wamejiandikisha kupiga kura kati ya idadi ya watu wapatao milioni 1.4.