Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in, apendekeza marufuku ya ulaji wa nyama ya mbwa

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in, amependekeza marufuku ya ulaji wa nyama ya mbwa nchini humo, akisema tamaduni hiyo imekuwa aibu kubwa kwa taifa hilo kwa miaka mingi.

Nyama ya mbwa imekuwa kati ya vyakula vinavyopendwa nchini Korea kusini ikiaminika kuwa mbwa milioni moja huliwa kila mwaka, ila ulaji wa nyama hiyo umekuwa ukipungua katika siku za hivi karibuni baada ya watu kuchukulia mbwa kama marafiki kuliko kitoweo.

Tamaduni hiyo imekuwa mwiko kati ya vijana na shinikizo kutoka kwa makundi ya kutetea haki za wanyama imefanya tamaduni hiyo kuanza kufifia.

“Naona ni wakati sasa tuanze kufikiria kuacha kula nyama ya mbwa?” Rais Moon alimuuliza Waziri mkuu Kim Boo-kyum, wakati wa mkutano wao wa kila wiki uliofanyika Jumatatu.

Sekta ya ufugaji wanyama kama marafiki inaongezeka Korea Kusini , ikiwa sasa watu wengi wanafuga mbwa kama rafiki, rais akiwa mmoja wa watu hao. Rais Moon anapenda mbwa sana na anajulikana kwa kuweka mbwa hata kwenye ikulu.

Rais Moon alisema haya baada ya kufahamishwa kuhusu mpango wa kuboresha utunzi wa wanyama waliotelekezwa, msemaji wake alisema.

Sheria ya Korea Kusini ya kuwalinda wanyama inalenga kuzuia uchinjaji wa kikatili wa mbwa na paka, ila haipingi ulaji wa mbwa.