Rais wa Malawi Lazarus Chakwera Jumatatu jioni alivunja baraza lake la mawaziri na kutoa “onyo kali” kwa mkuu wa kupambana na ufisadi ambaye alifichua wazi madai ya ufisadi ya kiwango cha juu kwenye mazungumzo ya simu yaliyovuja.
Chakwera aliyasema hayo katika hotuba yake ya taifa kupitia televisheni baada ya mazungumzo hayo kusambaa kwa kasi mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, Martha Chizuma alizungumzia baadhi ya kesi zilizo chini ya uchunguzi wa pamoja wa mashirika ya kupambana na rushwa ya Malawi na Uingereza, na kutilia shaka mafanikio yake upande wa mashtaka, ukisema vigogo wengi wamehongwa.
“Kwa kutumia mamlaka niliyopewa na Katiba, nimevunja Baraza langu lote la Mawaziri mara moja, na majukumu yote ya Baraza la Mawaziri yatarejea kwenye ofisi yangu hadi nitakapotangaza Baraza la Mawaziri lililoundwa upya baada ya siku mbili,” alisema Rais.
Chakwera pia alisema kwamba “haungi mkono msamaha uliotolewa kwa wale walioilaghai serikali na watu wa Malawi.”
Wakati huo huo, Chizuma alikiri kwamba matamshi yaliyovuja ni ya kweli.
“Nimedhamiria kuwa jambo zuri zaidi la kufanya katika kesi hii ni kuangalia kwa uangalifu mwenendo wake wa jumla wa shughuli za ofisi ili kuhakikisha kuwa hakuna matukio mengine ya wasiwasi juu ya jinsi anavyotekeleza kazi zake.” Chakwera alisema.
Malawi hivi majuzi imegonga vichwa vya habari tangu baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa kisiasa kushutumiwa kunufaika na mikataba inayomhusisha mfanyabiashara wa Malawi mwenye makazi yake nchini Uingereza.
Nchi hiyo ya Afrika Kusini ni mojawapo ya nchi maskini zaidi, ambazo bado zinakabiliwa na uhaba wa chakula, na imeathirika pakubwa na janga la UVIKO-19, kulingana na ripoti ya nchi ya 2021 ya Shirika la Fedha la Kimataifa IMF.