Rais wa Sri Lanka anayekabiliwa na mzozo aliondoka nchini mwake kwenda Maldives mapema Jumatano, ikiwa ni utangulizi wa kujiuzulu kwake baada ya miezi kadhaa ya maandamano kupinga mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi wa taifa lake la kisiwa kuwahi kutokea.
Gotabaya Rajapaksa alikuwa ameahidi mwishoni mwa juma kujiuzulu siku ya Jumatano na kufungua njia kwa ajili ya mabadiliko ya amani ya uongozi.
Akiwa rais, Rajapaksa ana kinga dhidi ya kukamatwa, na inaaminika alitaka kwenda nje ya nchi kabla ya kuondoka madarakani ili kuepusha uwezekano wa kuzuiliwa.
Yeye, mke wake na walinzi wawili walikuwa abiria wanne waliokuwa kwenye ndege ya kijeshi ya Antonov-32 iliyopaa kutoka uwanja mkuu wa kimataifa wa Sri Lanka, vyanzo vya uhamiaji viliiambia AFP.
Walipowasili Maldives, walipelekwa hadi eneo lisilojulikana chini ya ulinzi wa polisi, afisa wa uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Male alisema.
Raia wa Sri Lanka waliokuwa wakitabasamu walijazana tena kwenye korido za makazi rasmi ya rais baada ya kuondoka siku ya Jumatano, huku wapenzi wakitembea huku wakiwa wameshikana mikono katika hali ya kusherehekea kuondoka kwake.
“Watu wana furaha sana, kwa sababu watu hawa waliibia nchi yetu,” alisema mtumishi wa umma mstaafu Kingsley Samarakoon, 74. “Wameiba pesa nyingi sana, mabilioni na mabilioni.”
Lakini hakuwa na matumaini ya kuboreka mara moja kwa hali ya sasa ya Sri Lanka.
“Je, watu wataendeshaje nchi bila pesa?” Aliuliza. Ni tatizo.”
Kuondoka kwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 73 aliyejulikana kwa jina la “The Terminator” kulizuiliwa kwa zaidi ya saa 24 katika mvutano wa kufedhehesha na wafanyikazi wa uhamiaji huko Colombo.
Alikuwa akitaka kwenda hadi Dubai kwa ndege ya kibiashara, lakini wafanyakazi wa Bandaranaike International walijiondoa kwenye huduma za VIP na kusisitiza kwamba abiria wote walipaswa kupitia kaunta za umma.
Kundi la rais lilisita kupitia njia za kawaida, likiogopa hasira za umma, afisa wa usalama alisema, na kwa sababu hiyo, walikosa safari nne za ndege siku ya Jumatatu ambazo zingeweza kuwapeleka Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kibali cha ndege ya kijeshi kutua katika nchi jirani ya India hakikupatikana mara moja, afisa wa usalama alisema, na wakati mmoja Jumanne kundi hilo lilielekea kwenye kambi ya wanamaji kwa nia ya kukimbia kwa kutumia chombo cha bahari.
Kakake mdogo Rajapaksa, Basil, ambaye alijiuzulu mwezi Aprili kama waziri wa fedha, alikosa kusafiri kwa ndege ya shirika la Emirates kuelekea Dubai mapema Jumanne baada ya mzozo na wafanyakazi wa uwanja wa ndege.
Basil — ambaye ana uraia wa Marekani pamoja na Sri Lanka — alijaribu kutumia huduma ya malipo ya concierge kwa wasafiri wa biashara, lakini wafanyakazi wa uwanja wa ndege na uhamiaji walisema wamejiondoa kwenye huduma hiyo.
Ilimbidi Basil kupata pasipoti mpya ya Marekani baada ya kuacha yake katika ikulu ya rais wakati jamii hiyo ya Rajapaksa kuondoka kwa haraka ili kuepuka makundi ya watu waliojaribu kuwavamia siku ya Jumamosi, chanzo cha kidiplomasia kilisema.
Vyanzo rasmi vilisema begi lililojaa hati pia lilikuwa limeachwa nyuma katika jumba hilo la kifahari pamoja na rupia milioni 17.85 (kama dola 50,000) taslimu ambazo sasa ziko chini ya ulinzi wa mahakama ya Colombo.
Ofisi ya Waziri Mkuu ilithibitisha Jumatano kwamba Rajapaksa aliondoka nchini, lakini ilisema haina ratiba ya tangazo lolote la kujiuzulu kwake.
Rajapaksa anashutumiwa kwa kusimamia vibaya uchumi hadi kufikia hatua ambapo nchi hiyo imekosa fedha za kigeni kugharamia hata bidhaa muhimu zaidi kutoka nje, na kusababisha ugumu wa maisha kwa watu wake milioni 22.
Iwapo atang’atuka kama alivyoahidi, Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe atakuwa kaimu rais moja kwa moja hadi bunge litakapomchagua mbunge kuhudumu muhula wa urais, ambao utakamilika Novemba 2024. Lakini Wickremesinghe mwenyewe ametangaza nia yake ya kung’atuka iwapo makubaliano yatafikiwa kuhusu kuunda serikali ya umoja.
Mchakato wa urithi unaweza kuchukua kati ya siku tatu — muda wa chini zaidi kuchukuliwa kuitisha bunge — na upeo wa siku 30 unaoruhusiwa chini ya sheria.
Ikiwa Rajapaksa atajiuzulu Jumatano, kura itafanyika Julai 20, spika wa bunge amesema.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Samagi Jana Balawegaya, Sajith Premadasa, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa urais wa 2019 dhidi ya Rajapaksa, amesema atawania nafasi hiyo.
Premadasa ni mwanawe rais wa zamani Ranasinghe Premadasa, ambaye aliuawa katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga lililofanywa na waasi wa Kitamil mnamo Mei 1993.
Sri Lanka imeshindwa kulipa deni lake la nje la dola bilioni 51 mwezi Aprili na iko kwenye mazungumzo na IMF kwa uwezekano wa kupata dhamana.
Kisiwa hicho kimekaribia kumaliza akiba yake wa petroli ambayo tayari ni adimu.
Serikali imeagiza kufungwa kwa ofisi na shule zisizo za lazima ili kupunguza usafiri na kuokoa mafuta.