Kujiuzulu kwa rais wa Sri Lanka kumekubaliwa, spika wa bunge la nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo alitangaza Ijumaa, baada ya kutoroka nchini mapema wiki hii na kumjulisha kutoka Singapore kwamba anajiuzulu.
Tamko hilo rasmi linamfanya Gotabaya Rajapaksa — ambaye wakati mmoja alijulikana kama ‘The Terminator’ kwa kuwakandamiza kikatili waasi wa Kitamil — mkuu wa kwanza wa nchi ya Sri Lanka kujiuzulu tangu mwaka 1978.
Alituma barua pepe ya kujiuzulu kwake kutoka Singapore baada ya kusafiri kwa ndege kuenda Singapore kutoka Maldives, ambapo awali alitoroka baada ya waandamanaji kuvamia ikulu yake mwishoni mwa juma.
“Gotabaya amejiuzulu kihalali” kuanzia Alhamisi, spika Mahinda Yapa Abeywardana aliwaambia waandishi wa habari.
“Nimekubali kujiuzulu kwake.”
Chini ya katiba ya Sri Lanka, Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe — ambaye pia waandamanaji wanamtaka aondoke atakuwa kaimu rais hadi bunge litakapomchagua mbunge kuchukua nafasi ya Rajapaksa kuhudumu kwa muda uliosalia.
Bunge litaitishwa Jumamosi, Abeywardana aliwaambia waandishi wa habari katika makazi yake, na kuongeza kuwa anatumai kukamilisha mchakato wa uchaguzi ‘ndani ya siku saba.’
Kuondoka kwa Rajapaksa kulikuja baada ya miezi kadhaa ya maandamano juu ya kile wakosoaji walisema ni usimamizi mbovu wa uchumi wa kisiwa hicho, na kusababisha shida kubwa kwa watu wake milioni 22.
Katika uwanja ambao umetumika kama makao makuu ya vuguvugu la maandamano lililomwondoa madarakani, umati mdogo wa watu ulikusanyika Alhamisi kusherehekea kujiuzulu kwake.
Ni mamia tu ya watu waliokuwepo kuadhimisha hatua hiyo muhimu, huku maveterani wengi wa vuguvugu la maandamano wakiwa wamechoka baada ya kustahimili mashambulizi ya mabomu ya machozi na makabiliano makali na vikosi vya usalama katika siku zilizopita.
“Kwa hakika ninahisi, nadhani umati hapa hakika unahisi, una furaha kuhusu hilo,” mwanaharakati Vraie Balthaazar alisema.