Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewaita wabunge wa chama tawala kwenye mkutano Alhamisi kujadili sheria kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ambayo imekosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa na wanaharakati wa haki za binadamu.
Bunge mwezi uliopita liliidhinisha Mswada wa Kupinga Ushoga wa 2023, unaotaka adhabu kali kwa yeyote anayejihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Ridhaa ya Museveni inahitajika ili iwe sheria na imekabiliwa na miito mingi ya kukataa kile ambacho kimeshutumiwa kuwa miongoni mwa sheria kali zaidi duniani dhidi ya mashoga.
Chini ya mswada huo, mtu yeyote anayejihusisha na mapenzi ya jinsia moja anaweza kukabiliwa na kifungo cha maisha huku wanaorudia makosa hayo wakihukumiwa kifo, kulingana na wanaharakati.
Barua ilitumwa na kinara mkuu wa chama tawala cha National Resistance Movement kwa wabunge wa chama hicho akiwaalika kwenye mkutano Alhamisi katika makazi rasmi ya Museveni katika jiji la Entebbe ili “kujadili miongoni mwa (mambo) Mswada wa Kupinga Ushoga wa 2023”.
Mwezi uliopita, Ikulu ya White House ilionya Uganda juu ya uwezekano wa athari za kiuchumi ikiwa sheria hiyo itaanza kutekelezwa.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Turk pia alimtaka Museveni kutotangaza mswada huo kuwa sheria.
“Kupitishwa kwa mswada huu wa kibaguzi, pengine miongoni mwa mswada mbaya zaidi wa aina yake duniani, ni jambo linalosumbua sana,” alisema baada ya kura ya bunge ya Machi.
Lakini majirani wengi wa Uganda pia wanakandamiza haki za mashoga, huku wanasiasa nchini Kenya na Tanzania kwa mfano wakionya dhidi ya juhudi zozote za kuongeza ufahamu wa masuala ya LGBTQ.
Ushoga ulihalalishwa nchini Uganda chini ya sheria za enzi za ukoloni lakini tangu uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo 1962 hakujawa na hatia ya kufanya mapenzi ya jinsia moja.