Ibrahim Boubacar Keita, rais wa zamani wa Mali ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 76. Keita aliingia madarakani kwa ahadi ya uongozi mwadilifu lakini akaondolewa madarakani katika mapinduzi ya mwaka 2020 huku kukiwa na madai ya ufisadi. Keita alifariki Jumapili nyumbani kwake katika mji mkuu Bamako.
Kifo chake kilithibitishwa kwenye Twitter na Abdoulaye Diop, waziri wa zamani wa mambo ya nje, aliyekuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Mali.
Kilichosababisha kifo chake hakikuwekwa wazi. Bw. Keita kwa miaka mingi amekuwa akitafuta matibabu katika Umoja wa Falme za Kiarabu na alilazwa hospitalini mwezi Septemba muda mfupi baada ya kupinduliwa.
Bw. Keita, maarufu kwa jina IBK, alikuwa rais wa Mali kutoka 2013 hadi 2020, katika kipindi cha misukosuko katika historia ya hivi majuzi ya Mali.
Mapinduzi ya mwaka wa 2012 yalisababisha mzozo ambao ulimsaidia kushinda uchaguzi wa mwaka huo, mapinduzi mengine ya Agosti 2020 yalisababisha kukamatwa kwake na askari wenye silaha ambao walimlazimisha kujiuzulu kupitia televisheni, ila aliachiliwa huru baadaye.
Katika muda wake madarakani, ukosefu wa usalama uliongezeka zaidi nchini Mali.
Kupanda kwake madarakani mwaka 2013 kulifuatia mzozo ambapo viongozi wa mapinduzi walipindua serikali, kisha waasi wakaiteka miji ya kaskazini mwa Mali.
Waislam wenye msimamo mkali walitumia machafuko hayo, na kuweka uongozi wa Shariah katika miji ya Timbuktu, Gao na Kidal. Uingiliaji wa jeshi la Ufaransa, mtawala wa zamani wa kikoloni wa Mali, uliwafurusha wana itikadi wakali kutoka ngome zao za kaskazini, lakini tangu wakati huo ukosefu wa usalama umeenea katika eneo hilo.
Alipokuja uongozini, wananchi wengi wa Mali walimwona Bw. Keita, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu katika miaka ya 1990, kama mtu mwaminifu ambaye angeweza kuiongoza Mali kutoka katika mgogoro huo tata. Lakini sifa yake ilichafuliwa na tuhuma za ufisadi na upendeleo, na ikapelekea kupinduliwa kwake. Maandamano makubwa ya kupinga uchaguzi wa wabunge aliotuhumiwa kuiba kwa kuwasimamisha wagombea wake ulichangia kuondoka kwake madarakani.
Mwanawe Karim Keita, alivutia hasira zaidi. Rais alipopinduliwa, watu walivamia nyumba ya kifahari ya mwanawe huko Bamako na kuipora. Wananchi wa Mali waliwaona walioongoza mapinduzi kama mashujaa.
Mbali na mwanawe, Bw. Keita ameacha watoto wengine watatu na mkewe, Aminata Maïga Keita.
Wakati utawala wa kijeshi ulipopendekeza mwezi huu kuongeza muda wa mpito kabla ya uchaguzi mpya kufanyika, majirani wengi wa Mali huko Afrika Magharibi waliweka vikwazo vikali, wakiungwa mkono na madola ya Magharibi na Umoja wa Mataifa.
Siku ya Ijumaa, wananchi wa Mali walijitokeza kupinga vikwazo hivyo, lakini pia, wakiunga mkono utawala wa kijeshi.