Rais wa zamani wa Zambia Rupiah Banda alifariki siku ya Ijumaa akiwa na umri wa miaka 85 baada ya kuugua saratani ya utumbo mpana kwa muda mrefu, mtoto wake Andrew alisema.
Kiongozi wa nne wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika tangu ijjipatie uhuru kutoka kwa Uingereza alihudumu kwa miaka mitatu kuanzia 2008 – muda unaokumbukwa kwa ukuaji wa uchumi na tuhuma za ufisadi.
Banda alikuwa makamu wa rais wakati mtangulizi wake Levy Mwanawasa alipoaga dunia kutokana na kiharusi, na ndipo akapanda cheo na kuwa rais.
Lakini mwanadiplomasia huyo mkongwe alishindwa katika uchaguzi wa 2011, licha ya kusimamia ukuaji mkubwa wa uchumi wakati wa uongozi wake.
Uchumi wa Zambia ulipanuka katika kipindi kifupi cha urais wa Banda, hasa kutokana na kupanda kwa bei ya shaba na kuongezeka kwa uwekezaji kutoka China.
Aliendelea na ujenzi ulioanza chini ya Mwanawasa, akijenga barabara, hospitali na shule zilizohitajika sana.
Zambia ilirekodi ongezeko la ukuaji kwa asilimia 7.6 mwaka 2011, kutoka asilimia 6.4 mwaka uliopita, chini ya uongozi wa Banda.
Alitumai kuwa kuboreka kwa kiuchumi kungewashawishi wapiga kura kumuweka madarakani.
Wengi wa wakazi milioni 17.9 wa Zambia, hata hivyo, hawakufaidika na manufaa ya uchimbaji madini na ujenzi ulioshamiri.
Utajiri ulijilimbikizia mikononi mwa watu wachache huku tuhuma za ufisadi zikiibuka na kuharibu sifa yake.
Mnamo Septemba 2011, alishindwa uchaguzini na kiongozi wa upinzani Michael Sata.
Kumhusu Rupiah Banda
Banda alizaliwa Februari 19, 1937 katika mji mdogo wa Gwanda katika nchi jirani ya Zimbabwe, wakati huo ikijulikana kama koloni la Uingereza la Rhodesia ya Kusini.
Wazazi wake walikuwa wamehama kutoka nchi jirani ya Zambia, iliyokuwa Rhodesia Kaskazini, kutafuta kazi.
Banda alirejea katika nchi yake ya asili na baadaye kuendelea na masomo yake nchini Ethiopia na Sweden, na kupata shahada ya uchumi.
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Banda alianza kazi ya kidiplomasia huko Uropa.
Baadaye aliteuliwa kuwa balozi wa Misri, Amerika na Umoja wa Mataifa.
Banda alijiunga na siasa za nchi mwaka 1975, alipohudumu kwa muda mfupi kama waziri wa mambo ya nje na kisha waziri wa madini chini ya rais wa kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda.
Mwanachama wa muda mrefu wa Chama cha Kaunda cha United National Independence Party (UNIP), Banda pia alikuwa mfanyabiashara maarufu na shabiki mkubwa wa soka.
Aliongoza makampuni kadhaa ya serikali chini ya Kaunda na alikuwa mmiliki wa KB Davis, kampuni ambayo ilisambaza vifaa vya uchimbaji madini katika eneo la ukanda wa shaba la kaskazini-kati mwa Zambia.
Pia alijishughulisha na michezo na wakati mmoja aliwahi kuwa makamu wa rais wa Chama cha Soka cha Zambia.
Pamoja na mafanikio yake, Banda bado alijionyesha kuwa mtu wa watu.“Pamoja na uzoefu wangu wa kisiasa mimi pia ni mkulima,” aliiambia AFP katika mahojiano ya 2008.
“Najua athari inayoweza kutokea wakati mvua inachelewa kunyesha na wakati mazao yanapofeli.”
“Rafiki wa wezi”
Banda alikuwa amepanga kustaafu siasa na kumaliza miaka mingi ya ushirikiano na UNIP ili kuishi katika shamba moja katika wilaya ya Chipata mashariki mwa Zambia.
Lakini Mwanawasa alimrudisha kwenye siasa, na kumteua kama makamu wa rais wa Banda muda mfupi baada ya ushindi wake wa mwaka 2006 dhidi ya Sata.
Mwanawasa alipofariki miaka miwili baadaye, Banda aliwashinda wagombea wengine kumi na wawili kutoka chama tawala cha Movement for Multi-Party Democracy (MMD) kuchukua nafasi ya marehemu mkuu wa nchi.
Muda si mrefu alishutumiwa kwa kuwapa kandarasi za serikali watoto wake na kuzembea kwenye kampeni ya kupinga ufisadi uliokithiri wakati wa Mwanawasa.
Mwaka 2009, Banda alikataa kukata rufaa ya kuachiliwa kwa rais wa zamani Frederick Chiluba, aliyeshitakiwa kwa tuhuma za ubadhirifu chini ya mtangulizi wake.
Kisha akavunja kikosi kazi cha ufisadi cha Mwanawasa, jambo lililomfanya Sata amtaje kama ‘rafiki wa wezi.’
Banda alitangaza kuwa aligunduliwa na saratani ya utumbo mpana mwaka wa 2020.
Kabla hapo, alikuwa amemuoa tena Thandiwe Banda, mwalimu wa sayansi ya siasa aliyekuwa mdogo wake kwa umri kwa takriban miaka 40.
Banda alipoingia madarakani, alikua mke wa rais mdogo zaidi katika historia ya Zambia.