Rais Wiliam Ruto anaelekea London kutoa heshima za mwisho kwa Malkia

Rais wa Kenya William Ruto katika ubalozi wa Uingereza jijini Nairobi Septemba 14, 2022.

Rais wa tano wa taifa la Kenya William Ruto ameondoka nje ya nchi hiyo kwa mara ya kwanza kama rais leo jumapili akielekea Uingereza kuhudhuria mazishi ya malkia Elizabeth wa pili.

Mwanzo Tv imebaini kuwa kiongozi huyo wa taifa la Kenya akiondoka dakika chache baada ya saa mbili asubuhi ya leo.

Ziara hii inajiri wiki moja tu baada yake kuapishwa na kuchukua rasmi mikoba kama rais wa tano wa taifa hilo.

Kiongozi huyo wa Kenya anatarajiwa kuandaliwa dhifa na mfalme Charles watatu mara baada ya kuwasili Uingereza.

Kawaida rais anapokuwa katika ziara rasmi sawa na hii anapaswa kuandamana na baadhi ya mawaziri katika baraza lake la mawaziri ila hadi sasa rais huyo bado hajataja mawaziri ambao watahudumu katika serikali yake.

Rais Ruto ameandamana na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na maafisa katika wizara ya masuala ya kigeni..

Ruto atakuwa miongoni mwa wageni mashuhuri wa nchi za kigeni ambao watahudhuria mazishi ya Malkia wa Uingereza.

Rais William Ruto alipowasili katika Ubalozi wa Uingereza Jijini Nairobi.

Tayari rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Tanzania Samia Suluu Hassan na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese na Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinta Ardern wamefika London ili kuhudhuria mazishi hayo yatakayowakutanisha viongozi wengi wa ulimwengu.

Viongozi wengine wa Jumuiya ya Madola wanaotarajiwa kuhudhuria ni pamoja na Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina na Rais wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe.

Mkutano wa umoja wa mataifa (UNGA)

Baada ya mazishi, rais Ruto ataelekeza Marekani ambapo ameratibiwa kuhudhuria mkutano mkuu wa 77 wa umoja wa mataifa (UNGA) mjini New York.

Aidha rais Ruto vilevile anatarajiwa kukutana na rais wa Marekani Joe Biden.

Mkutano mkuu wa umoja wa mataifa utakuwa ndio mwanzo unaandaliwa ana kwa ana tangu ujio wa virusi vya Korana vilivyositisha mikutano ya kutagusana.

Mikutano ya UNGA mwaka wa 2020 na 2021yaliandaliwa mtandaoni.