Rais William Ruto Adinda Kuhudhuria Mazishi Ya Aliyekuwa Waziri Magoha.


Rais wa Kenya William Ruto Jumamosi hakuhudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri wa elimu Profesa George Magoha kaunti ya Siaya.


Magoha alifariki Januari 24 ,2022 akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi baada ya kuugua ugonjwa wa moyo.


Mazishi ya profesa Magoha yalihudhuriwa na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ambaye aliongoza waliokuwa maafisa wa serikali na viongozi wa mrengo wa upinzani Azimio-Oka.


Wakati Mazishi ya Magoha yalikuwa yanaendelea,Rais William Ruto alikuwa eneo la Naivasha kaunti ya Nakuru akiendesha kikao cha serikali ya kitaifa na zile za kaunti ambacho kilihudhuriwa na magavana.


Naibu Rais Rigathi Gachagua pia hakufika katika mazishi ya Marehemu Profesa George Magoha katika kijiji cha Uriri kaunti ya Siaya.


Risala za rambirambi za Rais William Ruto zilisomwa na waziri wa mawasilano na teknolojia Eliud Owalo.


Rais Ruto kupitia ujumbe huo alimuomboleza profesa Magoha kama mzalendo ambaye aliipenda nchi yake na kujituma zaidi kazini.


Alisema kuwa Magoha hangeruhusu utepetevu kazini na hakusita kuwakosa wakati akihudumu kama serikalini.


“Nitamkumbuka profesa Magoha kama msomi,mchapa kazi na mtu aliyependa ukweli na uwazi katika kila kitu alichokifanya,” Ruto alisema.


Rais Willian Ruto alisema kuwa chini ya uongozi wa aliyekuwa waziri Magoha,kulishuhudiwa maadiliko katika sekta ya elimu.


“Atakumbukwa zaidi kwa kusimamia utekelezwaji wa mtaala mpya wa CBC na hata kuweka mikakati kabambe ya kufanikisha elimu katika kipindi kigumu cha Covid-19.”alisema.