Rais William Ruto amemdhubutu Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kuandaa maandamao ya kitaifa.
Ruto alikuwa anamjibu Odinga ambaye aliipa serikali ya Rais Ruto makataa ya siku 14 kupunguza gharama ya maisha la sivyo ataandaa maandamano kote nchini Kenya.
Odinga alitangaza haya katika mkutano wa maombi ambao uliandaliwa katika bustani ya Jeevanjee jijini Nairobi Jumatano,Februari 22.
Waziri huyo mkuu wa zamani alisema kuwa “Wakenya wamechoka na serikali ya Kenya kwanza kuwaahadaa na ahadi zisizotimizika”
Akizungumza katika uzinduzi wa tume ya kusafisha mto Nairobi Jumatano,Februari 22,Rais William Ruto alisema serikali ya Kenya Kwanza haitakubali vitisho vya maandamano na kuwataka viongozi wa upinzani kuheshimu katiba.
“Wanatutishia na kuandaa maandamano. Wataandamana hadi wachoke maanake Kenya ni taifa ambalo linaongozwa kwa kufuata sheria na Katiba. Kila mkenya ana uhuru, hakuna aliye juu ya mwingine,” alisema rais Ruto.
“Kama rais nitahakikisha kuwa hakuna mkenya atakayekandamizwa .Hakuna mtu yeyote ambaye atatishia usalama wa taifa hili kupitia maandamano,” alisema Rais Ruto
“Nataka kuwaambia wenzangu katika upinzani ambao wanatumia vitisho kutaka kuingia katika serikali kwamba hawana nafasi,walikuwa na wakati wao wa kuwatumikia wakenya na ukatamatika,ni wakati wetu,” alisema Rais Ruto
Odinga katika mkutano wake alimtaka Rais william Ruto kupunguza bei vyakula,umeme na hata ushuru.
“Tumekuwa tukizungumzia kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula,umeme,mafuta na hata ushuru.Ni hali ambayo imechangia hata wanafunzi wengi kuwacha shule kutokana na wazazi wao kukosa karo,” alisema Odinga.