Rais William Ruto asifia Ford Foundation kwa kulinda demokrasia Kenya

Rais William Ruto amelilimbikizia sifa Shirika la Ford Foundation kwa kusaidia kulinda demokrasia nchini Kenya.

Matamshi yake yanakuja miezi michache baada serikali yake  kulishutumu shirika hilo kwa madai ya kufadhili maandamano ya vijana (Gen Z)  nchini kenya .

“Kenya inalishukuru Shirika la Ford Foundation kwa dhamira yake ya kulinda demokrasia yetu na kuunga mkono miito ya Kenya ya kufanyia mabadiliko taasisi za kiuchumi duniani, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na udhibiti wa teknolojia ya kisasa,” alisema Ruto alipokutana na Rais wa Ford Foundation Darren Walker mjini New York nchini Marekani.

Mnamo mwezi Julai mwaka huu, utawala wa rais William Ruto ulilinyoshea kidole cha lawama Shirika la Ford Foundation lenye makao yake nchini Marekani kwa kufadhili maandamano ya kuipinga serikali.

Wakati huo, vijana wa Gen Z walifanya maandamano kote nchini kupinga Mswada wa Fedha 2024 wakidai ulikusudia kuwakandamiza.

Shinikizo zao ziliulazimu utawala wa Kenya Kwanza kufutilia mbali mswada huo. Aidha, vijana hao walishinikiza kufanywa kwa mageuzi mbalimbali nchini, hali ambayo serikali iliitikia kwa kuvunja Baraza la Mawaziri.

 

Ford Foundation ilikanusha vikali madai ya kufadhili maandamano hayo.

Katika taarifa walioitoa kwenye mtandao wao wakati huo, Ford Foundation ilisema, “Ingawa tunatambua haki ya Wakenya kutetea kwa amani nchi yenye haki na usawa, tunakanusha vitendo au matamshi yoyote ambayo yana chuki au kuunga mkono unyanyasaji dhidi ya taasisi yoyote, mtu binafsi au jamii yoyote. Hatukufadhili maandamano ya hivi majuzi dhidi ya mswada wa fedha na tuna sera isiyopendelea upande wowote kwa utoaji wetu wote wa ruzuku.”

 

Shirika la Ford ni la kibinafsi lililoanzishwa mwaka 1963 na Edsel Ford, mtoto wa mwanzilishi wa Kampuni ya Ford Motor Henry Ford.

 

Shirika hilo linalenga kuendeleza haki na maadili ya demokrasia na linaendesha shughuli zake duniani kote.