Rigobert Song kuteuliwa kuwa kocha wa Cameroon kwa amri ya rais wa taifa hilo

Rigobert Song,Mchezaji wa zamani wa Cameroon

Mchezaji nyota wa zamani Rigobert Song anatarajiwa kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Cameroon, akichukua nafasi ya Toni Conceicao, kwa amri ya rais wa nchi hiyo, waziri wa michezo alisema Jumatatu.

Conceicao raia wa Ureno imeiongoza Cameroon katika mechi ya mchujo ya kufuzu kwa Kombe la Dunia na kuifikisha katika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi uliopita.

Waziri wa michezo Narcisse Mouelle Kombi alisema Rais wa Cameroon Paul Biya ameamuru shirikisho la soka la kitaifa kumpa kazi mlinzi huyo wa zamani wa Liverpool.

“Kwa maagizo kutoka kwa Rais wa Jamhuri, kocha wa timu ya taifa ya soka ya wanaume, Bw Antonio Conceicao, amebadilishwa na Rigobert Song,” Kombi alisema katika taarifa.

“Shirikisho la Soka la Cameroon (Fecafoot) limealikwa kuchukua hatua zinazohitajika kwa utekelezaji wa haraka na wa usawa wa maagizo hayo.”

Fecafoot imethibitisha ‘mwisho wa mkataba wake’ na Conceicao.

Cameroon itamenyana na mabingwa wa Afrika wa mwaka wa 2019, Algeria katika mchezo wa hatua ya muondoano ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Qatar baadaye mwaka huu Machi 25 na 29.

Song, ambaye alicheza Uingereza, Ufaransa, Italia, Ujerumani na Uturuki wakati kabla kustaafu , ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Indomitable Lions akiwa na mabao 137.

Alicheza katika Kombe la Dunia mara nne na kushinda mataji ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya 2000 na 2002.

Song pia alikuwa mkufunzi wa timu ya vijana ya chini ya miaka 21 ya Cameroon.