Rais William Ruto ametangaza kwamba usajili wa kwanza wa wakenya walio na ujuzi katika fani mbali mbali watakaokwenda kufanya kazi nchini Ujerumani utafanyika tarehe 27 mwezi huu wa Septemba.
Akizungumza jana alipohudhuria ibada katika kanisa la Stewards Revival Pentecostal kaunti ya Nairobi, Rais aliwakaripia wakosoaji wa mapatano kati ya Kenya na Ujerumani kuhusu leba akisema wakenya wengi sasa watapata fursa ya kufanya kazi ughaibuni.
Rais Ruto alirejea Kenya jumapili asubuhi baada ya ziara ya siku tatu nchini Ujerumani.
“Niliposema wakenya watapata nafasi za kazi nchini Ujerumani, wengine hawakuniamini, lakini siku ya Ijumaa waliona mpango wetu ukitekelezwa. Baadhi ya Wakenya tayari wamewasili na tarehe 27 Septemba, tutakuwa na uajiri wa kwanza.” alisema kiongozi wa nchi.
Alitoa hakikisho kwamba ahadi za serikali ya Kenya Kwanza sio maneno matupu na akasisitiza dhamira ya utawala wake ya kutimiza malengo yake licha ya changamoto zinazoikabili.
“Tunatembea kwa imani kwa sababu tunaona uwezekano. Baadhi ya watu hawanielewi kwa sababu hawana maono hayo.” aliendelea kusema Rais Ruto.
Makubaliano ya wafanyikazi na Ujerumani yalijadiliwa kwa mara ya kwanza wakati wa ziara ya chansela wa Ujerumani Olaf Scholz nchini Kenya Mei, 2023.
Ingawa idadi kamili ya Wakenya ambao watahamia Ujerumani chini ya mpango huo bado haijulikani, mamlaka ya Ujerumani imetupilia mbali madai kwamba wafanyakazi 250,000 wataajiriwa.