Rwanda inajiandaa kuwakaribisha viongozi wa mataifa 54 kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola Ijumaa katika mji mkuu, Kigali.
Jumuiya ya Madola iliundwa mnamo 1931 baada ya Milki ya Uingereza kuanza kuvunjika na mataifa kudai uhuru wao.
Lengo lake ni kufanyia kazi malengo ya pamoja ya ustawi, demokrasia na amani.
Rwanda na nchi nyingine nne si koloni za zamani za Uingereza.
Mkutano wa kilele wa wiki hii, ambao umeahirishwa mara mbili tangu 2020 kutokana na janga la coronavirus, unagubikwa na wasiwasi juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Rwanda na mipango ya Uingereza ya kutuma waomba hifadhi katika taifa hilo la Afrika.
“Serikali ya Rwanda imekuwa na azma ya kuwa na mkutano wa ana kwa ana ili iweze kuonyesha nchi na kuonyesha mji mkuu,” anasema Profesa Philip Murphy, mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Jumuiya ya Madola katika Chuo Kikuu cha London.
Rais wa Rwanda Paul Kagame “anataka aina ya sifa za kuhusishwa na shirika linalodai kuwa linazingatia maadili, linadai kwamba linaunga mkono haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria … Na ni wazi kuwa yeye ni mtu mwenye utata sana. Rekodi ya haki za binadamu ya Rwanda inatia shaka na ni yenye utata.”
Rwanda inakanusha kuwa serikali inakiuka haki za binadamu.
Wafuasi wa Kagame wanasema kuandaa mkutano wa Jumuiya ya Madola ni hatua nyingine muhimu katika maendeleo ya haraka ya nchi tangu mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambapo takriban watu 800,000 waliuawa.
Mapema mwaka huu, Uingereza ilitia saini mkataba na serikali ya Rwanda kuwahamisha waomba hifadhi wanaowasili katika ufuo wake hadi nchini Rwanda.
Ndege ya kwanza ilipaswa kuondoka wiki jana lakini ilizuiwa dakika chache kabla ya kupaa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.
Wakosoaji wanasema sera hiyo inakiuka sheria ya wakimbizi.
Serikali ya Uingereza inasema sera hiyo ni halali na itawazuia wahamiaji haramu.
“Watu wanapokuja hapa kinyume cha sheria, wanapovunja sheria, ni muhimu tuweke tofauti hiyo. Hilo ndilo tunalofanya na sera yetu ya Rwanda,” Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson aliwaambia waandishi wa habari Juni 18.
Uingereza imekuwa na uhusiano wa karibu na Rwanda tangu nchi hiyo ilipojiunga na Jumuiya ya Madola mwaka 2009.