Rwanda siku ya Jumatatu ilifungua tena mpaka wake wa ardhini na Uganda baada ya kufungwa kwa miaka mitatu, kuashiria kuwa uhusiano kati ya majirani hao wawili wa Afrika Mashariki umeimarika tena.
Mpaka huo ulifungwa Februari 2019 baada ya mvutano wa kisiasa kati ya Kigali na Kampala ulipozidi, na kusababisha kukaribia kuporomoka kwa biashara katika mataifa hayo mawili.
Rwanda ilitangaza uamuzi wake wa kufungua tena mpaka wiki iliyopita kama hatua ya kurekebisha uhusiano kati yake na Uganda ambao ulikuwa umesambaratika kutokana na shutuma mbalimbali za ujasusi, utekaji nyara na kuingilia kati serikali ya Uganda.
Kufunguliwa tena kwa mpaka huo kulifuatia ziara ya mwanawe wa kiume wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni Muhoozi Kainerugaba nchini Rwanda ambapo alikutana na Rais wa Rwanda Paul Kagame.
Kivuko cha Gatuna, kinachojulikana kama Katuna nchini Uganda, kilifunguliwa rasmi usiku wa manane, na msongamano wa magari ulitarajiwa kuongezeka kwa kasi siku nzima.
Museveni na Kagame walikuwa washirika wa karibu miaka ya 1980 na 1990 wakati wa vita vya kugombea madaraka katika nchi zao, lakini mahusiano yaligeuka kuwa ya uhasama mkubwa katika miaka ya hivi karibuni.
Rwanda ilifunga mipaka yake baada ya kuishutumu Uganda kwa kuwateka nyara raia wake na kuwaunga mkono waasi wanaotaka kumpindua Kagame.
Uganda nayo iliishutumu Rwanda kwa kufanya ujasusi na kuwaua wanaume wawili wakati wa uvamizi nchini Uganda mnamo 2019 – madai ambayo Kigali ilikanusha.
Serikali zote mbili zilisema wiki iliyopita zinatumai kufunguliwa tena kwa mpaka kunaweza kuboresha uhusianokati ya mataifa hayo mawili.
Kabla ya kufungwa, mauzo ya Uganda kwenda Rwanda — hasa saruji na chakula – yalikuwa yamefika kiasi cha zaidi ya dola milioni 211 mwaka 2018, kulingana na takwimu za Benki ya Dunia, wakati Rwanda iliuza bidhaa za thamani ya dola milioni 13 kwenda Uganda.
Biashara katika mataifa hayi ilishuka mnamo 2019, huku hali hiyo pia ikichangiwa na kulipuka kwa janga la UVIKO 19.