Sasa ni bayana kuwa sajili ya kuchapisha pia itatumika katika zoezi la uchaguzi kinyume na jinsi tume ya IEBC ilivyokuwa imeshikilia. Jaji wa mahakama Kuu Mugure Thande katika uamuzi wake ameshinikiza tume hiyo itumie sajili hiyo kama njia mbadala.
Mahakama kuu nchini Kenya imeaamuru Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi ya taifa hilo (IEBC) kutumia sajili iliyochapishwa wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Jaji Mugure Thande katika uamuzi wake ametupilia mbali uamuzi wa tume hiyo ya IEBC kutotumia sajili ya daftari ya wapiga kura na wakati huohuo kuondolea mbali barua iliyoandikwa na tume hiyo kwa muungano wa Azimio wakisema watatumia sajili ya kielectroniki pekee.
Jaji Mugure amesema hatua hiyo inakwenda kinyume na katiba ya Kenya na kuamrisha IEBC kutumia daftari la wapigakura kuwatambua wapiga kura.
“Nini kitakachotokea kwa mpiga kura aliyejiandikisha ambaye maelezo yake hayapatikani katika mitambo ya KIEMS kutokana na kufeli kwa teknolojia iwapo sajili ya iliyochapishwa haitakumika?” aliuliza Jaji Mugure.
Jaji huyo amesisitiza kuwa hatua ya IEBC kutotumia sajili iliyochapishwa inakiuka masharti ya katiba ya Kenya ambayo inaelekeza kuwa pale ambapo mtambo ya kieletroniki unapofeli basi sajili ya madaftari itumike.
Katika uamuzi huo Jaji huyo amesema iwapo msimamo wa IEBC ungekubaliwa basi wapiga kura wengi wangenyimwa haki yao ya kikatiba ya kushiriki katika zoezi muhimu la kuwachagua viongozi wao ilioko katika kipengele cha 38b cha katika ya Kenya.
Jaji huo vilevile ameongeza ingawaje tume ya IEBC haikutenda hayo kwa ukaidi au uovu, lakini ilikiuka katiba na sheria.
“Kwa kutumia sajili ya kielektroniki pekee kuna hatari ya kutowapa baadhi ya wakenya wapigakura nafasi ya kupiga kura, korti hii hivyo basi sharti iingilie kati kupitia mamlaka yake ya usimamizi kuhakikisha kwamba tume kutokana na uhuru wake inafanya kazi kwa kuzingatia katiba.”
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na makundi ya wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu kwa misingi kwamba mitambo ya teknolojia hukumbwa na matatizo ya mara kwa mara, hivyo njia mbadala ilifaa kuwa sajili iliyochapishwa.