Samia Amkaba Ruto Hadharani Kuhusu Refinery ya Tanga

Ziara ya kiserikali ya Rais wa Kenya William Ruto nchini Tanzania tarehe 5 Mei imezaa makubaliano kadhaa ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili lakini pia imeibua maswali nyumbani Kenya.

Ziara hiyo ililenga kuimarisha uhusiano kati ya Nairobi na Dar es Salaam, huku viongozi hao wakishuhudia kusainiwa kwa makubaliano katika sekta muhimu kama nishati, usafiri, biashara, utalii na usalama, pia walikubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi katika biashara ifikapo tarehe 30 Juni, hatua inayotarajiwa kurahisisha biashara kati ya mataifa hayo.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Rais Samia Suluhu Hassan alimhoji hadharani Rais Ruto kuhusu tangazo lake la awali kuhusu mpango wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta (refinery) huko Tanga, akisema hakuwa na taarifa nalo. “Tulipokuwa tunaongea ndani kule, nilimbana Ruto nikamwambia, umekwenda kutangaza refinery Tanga, mbona mimi sijui?” alisema.

Kwa upande wake, Ruto alieleza kuwa wazo la refinery bado liko katika mazungumzo na halijafikiwa makubaliano ya mwisho. Alisema miradi kama hiyo itajadiliwa na kutekelezwa kwa ushirikiano na Tanzania, pia alijaribu kupunguza mvutano huo kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

“Tunaihitaji kila mmoja… kadri tunavyolitambua hilo mapema, ndivyo tutakavyoweza kuepuka mashaka yasiyo ya lazima kati ya nchi zetu,” alisema.

Mbali na tukio hilo, viongozi hao walieleza dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano wa kikanda. Hii inajumuisha mipango ya kuboresha miundombinu ya reli kati ya Tanzania na Kenya, pamoja na mazungumzo kuhusu miradi ya nishati ikiwemo uwezekano wa bomba la gesi kati ya Dar es Salaam na Mombasa. Masuala ya usalama wa mipakani pia yalijadiliwa, huku pande zote zikikubaliana kuimarisha ushirikiano ili kudhibiti uhalifu wa kuvuka mipaka.

 

Licha ya kuonekana kwa mshikamano huo, ziara hiyo imekosolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini Kenya chini ya kundi la Linda Mwananchi. Katika taarifa yao, kundi hilo lilihoji muda na lengo la ziara hiyo, likisema hotuba iliyopangwa ya Rais Ruto katika Bunge la Tanzania inaweza kutafsiriwa kama kuunga mkono serikali inayokosolewa kuhusu masuala ya demokrasia, hasa baada ya uchaguzi wa mwaka 2025.

Pia walitaka uwazi kuhusu faida za ziara hiyo kwa wananchi wa Kenya, wakisema serikali inapaswa kuangazia zaidi masuala kama gharama ya maisha, ukosefu wa ajira na imani ya umma kwa uongozi.

Hata hivyo, serikali zote mbili zimeendelea kusisitiza kuwa ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hasa katika biashara, miundombinu na maendeleo ya pamoja.